Serikali kusimamia mazishi, mwili kutosafirishwa,
RC: lini na wapi si muhimu sana, watu wachache ndio watakaoshiriki
Na Penina Malundo,
WATU wasiozidi 10 wanatarajia kushiriki mazishi ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Evod Mmanda aliyefariki juzi saa 5 usiku katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara Ligula baada ya kuugua kwa muda mfupi.
Kupitia taarifa yake fupi kwa wananchi Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa alisema wamekubaliana na familia kwamba Serikali ndiyo itakayosimamia mazishi yake na hakutakuwa na kusafirisha mwili.
“Mazishi yatafanyika hapa Mtwara na hayatahudhuriwa na watu zaidi ya 10,” alisema Byakanwa wakati akieleza utaratibu wa mazishi ya DC Mmanda na kuongeza;
“Na ni katika msisitizo ule ule wa kuzuia msongamano na mkusanyiko. Nishukuru familia na ndugu wa marehemu tumekubaliana. Ni lini na wapi si muhimu sana kwa sababu itawahusu hao watu wachache watakaoshiriki.”
Alisema ni kipindi kigumu sana lakini anashukuru wao (familia) Serikali inapata ushirikiano mzuri sana kutoka kwa familia yake na wanasubiri wafike.
Alisema wameishakubaliana idadi ya watu wanaotakiwa kufika Mtwara ili kushiriki mazishi hayo.
“Kwa wana Mtwara, wana CCM na kwa watumishi nitoe pole kwamba tumeondokewa na kiongozi na mchapa kazi,”alisema.
Kifo cha DC Mmanda kimethibitishwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais — TAMISEMI, Seleman Jafo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Rebecca Kwandu.
Kupitia taarifa hiyo, Waziri Jafo alisema; “Nasikitika kutangaza kifo cha Mheshimiwa Avod Herman Mmanda, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, kilichotokca jana (juzi Aprili 26) saa 5:00 usiku katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mtwara baada ya kuugua kwa muda mfupi.”
Waziri Jafo alisema Serikali itamkumbuka kwa kuenzi mchango wa Marehemu Mmanda.
Alisema Mmanda alifanya kazi katika maeneo mbalimbali nchini hadi alipoteuliwa na Rais wa John Magufuli kushika nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Desemba 19, 2016. Mchango wake katika Taifa utaendelea kukumbukwa.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Mmanda ambaye ni alikuwa wakili wa kujitegemea kabla ya kifo chake aliwahi kulazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) miezi minne iliyopita na kuruhusiwa baada ya afya yake kuimarika.
Wakili Msomi Mmanda aliyewahi kuwa pia mjumbe wa Bunge la Katiba. Katika Bunge hilo, akiteuliwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa muda wa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, Pandu Ameir Kificho, kama mmoja ya wajumbe 20 waliopewa jukumu la kumshauri ili kuboresha utendaji.
Mwaka 2015 Mmanda alitangaza nia ya kugombea ubunge jimbo la Rombo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) lakini kura hazikutosha.
Mwenyekiti wa Wakuu wa wilaya nchini, Daniel Chongolo kwa niaba ya Wakauu wa Wilaya alitoa pole nyingi kwa Rais John Magufuli, viongozi wote akiwemo Waziri Jofo kufuatia kifo hicho cha Mmanda.
Katibu wa wakuu wa wilaya nchini, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah, alitoa pole kwa wananchi wa Mtwara na wakuu wote wa wilaya kufuatia kifo cha DC Mmanda.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam