December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC wa Mkuranga ampokea Zitto Kabwe

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

HISTORIA ya maridhiano yaliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan imezidi kuandikwa baada ya msafari wa Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo,Zitto Kabwe kupokelewa na Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Khadija Nasiri Ali akiwa safarini kuelekea Wilaya ya Ikwiriri kwa ajili ya mkutano wa hadhara.

Zitto alipokelewa na mkuu huyo wa wilaya jana na kusema maridhiano yanayoendelea nchini yataifikisha Tanzania katika nchi ya asali na maziwa ikiwa kila mmoja atatimiza wajibu wake katika maridhiano hayo.

Alisema wanasiasa wanapaswa kukosoana kwa hoja zitakazojenga umoja wa kitaifa badala ya kubomoa umoja huo na kumtaka mkuu wa wilaya hiyo kuendeleza hali hiyo kwa wanasiasa wengine pasipo kujali nafasi na udogo wa vyama vyao.

Alitumia nafasi hiyo ya mapokezi kumtaka Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga kuhakikisha haki za watu anaowaongoza zinatekelezwa bila ubaguzi wa kisiasa kijinsia na kikabila kwa kile alichoeleza watanzania wote wana haki sawa popote wanapokuwa ndani ya nchi

“Napenda kumshukuru mkuu wa wilaya na timu yake kwa mapokezi haya ya heshima na hii ni ishara ya namna gani sisa za nchi yetu zimebadilika kama alivyosema Rais Samia Suluhu kule Arusha,siasa siyo uadui zamani ilikuwa ni nadra wanasiasa wa upinzani yupo kwenye ziara ya kueneza chama chake halafu mkuu wa wilaya na timu yake wanampokea”alisema Zitto

Akizungumzia sababu ya kuwapokea wanasiasa hao wakati huu, mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Nasiri alisema viongozi wa wilaya ya Mkuranga wanafahamu kazi na wajibu wa viongozi wa vyama vya siasa katika kazi na majukumu waliyojipangia katika wilaya hiyo yanalenga kujenga mustakabali wa Mkuranga

Aliongeza kuwa mbali na kutambua majukumu yao pia suala zima la ulinzi na usalama wa viongozi wa kisiasa na kiserikali wanapoingia katika wilaya hiyo ni lazima iwe ni jukumu lao mpaka watakapoondoka katika eneo lao

“Mbali ya wao kuwa wanasiasa wanaotokana na vyama vya upinzani lakini malengo makubwa ya vyama vya siasa,wanasiasa na kazi zao katika eneo letu la mkuranga tunaamini ni kuijenga mkurangaa katika mustabali mwema”alisema Mkuu huyo wa wilaya.

Akiwa katika wilaya ya Rufiji eneo la Ikwiriri, msemaji wa Sekta ya Mambo ya ndani wa Chama hicho, Mbarala Maharagande, alisema eneo la Ikwiriri linapaswa kurudishwa katika hali ya amani kama ilivyokuwa kabla yam waka 2017

Alisema matukio yaliyotokea mwaka 2017 yameacha majeraha makubwa kwa wananchi mbali mbali wa wilaya hiyo ikiwemo vifo vya ndugu zao ulemavu na mateso ya iakili kwa baadhi ya watu

“Tunataka uchunguzi wa kina ufanyike kwa matukio yote ya Ikwiriri na Mkuranga mwaka 2017 maarufu kwa jina la MKIRU,uchunguzi ufanyike waliokosea wawajibishwe na waliodhurika wafidiwe”alisema Maharagande.

Mkuu wa wilaya ya Mkuranga Khadija Nasiri Ali(mwenye kilemba Cheusi),akimsikiliza kiongozi wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe baada ya kupokewa na viongozi hao wa wilaya akiwa njiani kuelekea Ikwiriri kwenye mkutano wa Hadhara