Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
MKUU wa Wilaya ya Uyui mkoani Tabora, Mohamed Mtulyakwaku ameipongeza Kampuni ya Mawasiliano Yas kwa kujitolea kusogeza huduma za kidijitali na kifedha karibu zaidi na wananchi wa Tabora, kufuatia uzinduzi rasmi wa duka jipya la kisasa la Yas katika mkoa huo.
Duka hilo limezinduliwa kama sehemu ya mkakati wa kitaifa wa upanuzi wa Kampuni ya Yas, likiwa na lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano, kifedha na kidijitali kwa gharama nafuu katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Matiko Chacha, Mkuu wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa mashirika kama Yas katika kuwezesha ushirikishwaji wa kidijitali na ukuaji wa uchumi.
“Serikali ya Mkoa wa Tabora inatambua na kuthamini juhudi za Yas za kupanua huduma muhimu za mawasiliano na kifedha. Duka hili si tu kituo cha huduma, bali ni lango la fursa kwa wananchi wa Tabora.
“Litawarahisishia maisha yao ya kila siku na kuwafungulia milango ya uwezeshaji kiuchumi,” amesema Mtulyakwaku.
Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja na Uendeshaji wa Yas, Mwangaza Matotola, amesisitiza dhamira ya kampuni ya kuwawezesha Watanzania kupitia teknolojia inayopatikana kwa urahisi na inayokidhi mahitaji yao.
“Kupitia duka hili jipya la Yas hapa Tabora, tunathibitisha dhamira yetu ya kufikisha teknolojia pale inapohitajika zaidi.

“Lengo letu ni kuwaunga mkono vijana, wajasiriamali na kila Mtanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali. Yas na Mixx by Yas tunajivunia kuwa washirika wa kweli katika safari hii,” amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kanda ya Kati wa Yas, Said Idd, ameeleza kuwa duka hilo litatolewa huduma mbalimbali zikiwemo usajili wa laini za simu, huduma za kifedha kupitia Mixx by Yas.
Pia, uuzaji wa vifaa vya mawasiliano (routers, Mifi, na simu janja za Simujanja), pamoja na msaada maalum kwa wafanyabiashara kupitia suluhisho la Mjasiriamali Box.
Aidha, amebainisha kuwa mabadiliko ya majina ya biashara kutoka Tigo na Tigo Pesa hadi Yas na Mixx by Yas ni ishara ya dhamira pana ya kuleta ubunifu, kuwawezesha wateja na kushirikiana na jamii kwa karibu zaidi.

“Tabora ina nafasi muhimu katika mustakabali wa kidijitali wa Tanzania. Tunajivunia kuunga mkono mustakabali huo kwa kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi,” ameongeza Idd.
Uzinduzi huo pia uliashiria mwendelezo wa kampeni ya kitaifa ya Yas, “Anzia Ulipo”, wito thabiti unaohamasisha Watanzania kuanza safari yao ya mafanikio kwa kile walichonacho, popote walipo.
Kampeni hiyo inaangazia nafasi ya Yas kama mshirika wa maendeleo katika jamii inayozidi kuunganishwa kwa njia ya kidijitali.

Kwa sasa, Yas ina jumla ya matawi manane yanayofanya kazi katika mkoa wa Tabora, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kitaifa za kuwekeza katika kupanua upatikanaji wa huduma na kuendeleza ujumuishaji wa kifedha na kidijitali nchini kote.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi