Na Mwandishi Wetu, timesmajira
MKUU wa Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro, Shaka Hamdu Shaka, ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa mradi wa ujenzi wa jengo la wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali ya Wilaya hiyo lililogharimu Sh. milioni 278 ambalo ujenzi wake umeonekana kuwa chini ya viwango kabla ya kuanza kutumika.
Akizungumza na watumishi na viongozi wa Hospital hiyo mara baada kutembelea na kukagua jengo hilo kwa mara ya pili mwishoni mwa wiki, Shaka alisema ameshangazwa kukuta mradi huo umejengwa chini ya viwango ukiwa na mapungufu mengi na kuagiza marekebisho yafanyike mpaka sasa wameshindwa kukamilisha kwa wakati bila sababu za msingi.
“Fedha zimeletwa zaidi ya Sh. milioni 200 katika mradi huu lakini cha kusikitisha viongozi mmeshimdwa kujitambua, umakini na kusimamia jukumu hili, pamoja na yote mnaniambia hata mjenzi wa awali mliyempa kazi na kuharibu hamumjui mtampata wapi, mambo ya ajabu sana, haiwezekani kabisa ndio maana ninataka vyombo vyote vya ulinzi na usalama vilivyopo hapa kila chombo kibebe jukumu lake nataka nipatiwe taarifa ya uchunguzi na watafutwe kila aliyehusika kwenye uzembe huu ifikapo Jumatano,”amesema Shaka na kuongeza kuwa:
“Nielezwe ni nini kinachoendelea TAKUKURU mpo hapa, jeshi la polisi mpo hapa na vyombo vingine kila mmoja afanye jukumu lake itakavyofika Jumatano ninataka taarifa tumechoka hizi hadithi ukienda ukirudi unapatiwa hadithi nyingine embu angalia kile nini? msicheze na fedha ya Serikali nia ya moto,”
Shaka ameshangazwa na jinsi ambavyo vifaa vilivyotumika katika jengo hilo kuwa vya kuunga unga na vyengine vikikosa ubora, uimara pamoja kuweka saruji katika paa za jengo hilo jambo ambalo limesabisha jengo hilo kuvujisha na maji kuingia ndani kuharibu taswira ya jengo.
“Ina maana huyu ameenda dukani kuomba vipande vipande mikanda ya gpsum ndio amekuja kutuwekea hapa, huwezi kusema hii mikanda imekuja kwenye jengo la serikali alafu kafanya hivi kwa jengo nzima viongozi mpo mnangalia mnaona ni sawa tu kuna shida hapa,” amesema Shaka
Amesema hajakubaliana na ujenzi wa mradi huo licha ya kuelezwa ni ICU wanayoitegemea, hivyo yoyote atakayebainika kucheza katika uzembe huo atawajibishwa.
“Dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan kuleta fedha hizi ni kusaidia jamii katika changamoto za kiafya hasa kwenye eneo hili nyeti na dharura, nataka niwaambie ndugu zangu kwenye hili tukibaini kuna uzembe wowote na kwa kila anayehusika kwa namna mmoja ama nyingine hatutasita kumchukulia hatua kali za kisheri sina masihara kwenye kusimamia dhamira ya Rais kwa wananchi wake ”
Aidha, Shaka alisema timu ya vyombo vya ulinzi na Usalama huku akiwasisitiza Takukuru itafanya uchunguzi na ripoti itawasilishwa mbele ya kamati ya ulinzi na usalama kwa ajili ya kufanyia kazi haraka iwezekavvyo ili wakati hatua zikichukuliwa ukarabati wa jengo uendelee na kuanza kutoa huduma mapema Aprili mwaka huu.
“Kama kuna kamati ama nani kahusika na huu uzembe kila mmoja akajitathimini mapema anatosha kwenye dhamana aliyopewa…vinginevyo sina msalie mtume, mradi huu tunauweka chini ya uangalizi kuanzia sasa tunaunda kamati ndogo itakayosimamia ujenzi, ukarabati na marekebisho mpaka yakamilike, nilikuja mara ya kwanza nikatoa maelekezo leo mnaniletea hadithi mapya hapana… hapana.. hapana hatutaki maneno tunataka huduma kwa wananchi” alisema Shaka.
Jengo la wagonjwa mahututi katika Hospital ya Wilaya ya Kilosa linajengwa kwa gharama za Sh. 280,000,000 kutoka serikali kuu ambapo fedha zimekwisha ujenzi huo umeonekana kuwa na mapungufu na kusababisha kuanza kutumia fedha kutoka mfuko wa hospitali ili kukamilisha ukarabati huo.
“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya tukiri mapungufu haya ni kweli tulipokea maelekezo yako lakini mie sio msemaji sana ila tulimtafuta fundi aliyepewa kazi tukamkosa hatukumpata na kulazimika kutafuta fundi mwingine ambae ndie huyu anaendelea na kazi kwa kutumia fedha za hospitali baada za awali kumalizika” Kaimu mganga mkuu wa Wilaya ya Kilosa Dk. John kiara
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu