November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Mpogolo:Dar es Salaam Sekondari iendane na hadhi ya Jiji

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online. Dar

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameagiza jengo la ghorofa lililokaa kwa muda mrefu takribani zaidi ya miaka isiyopungua 10, lililo katika shule ya Sekondari ya Dar es Salaam, kufanyiwa tathmini, ili kubaini kama linaweza kuendelezwa au kubomolewa na kujengwa jengo lingine litakaloendana na hadhi ya Jiji la Dar es Salaam.

Mpogolo ameyasema hayo Machi 19, 2024, alipotembelea katika Shule ya Sekondari ya Dar es Salaam, akiwa ameambatana na Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mussa Ally, ikiwa ni siku ya kumbukizi ya miaka mitatu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, tangu aingie madarakani, huku lengo la kutembelea shule hiyo likiwa ni kukagua viti na meza vilivyotengenezwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Amesema, lengo la kutembelea katika shule hiyo ni muendelezo wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo upande wa elimu, ikiwa pamoja na kuendana na kasi ya ukamilishaji wa madarasa na vifaa vya kusomea, kama viti na meza katika shule zote za sekondari wilayani humo, huku akitaja zaidi ya bilioni 24, kuwa zimetolewa na Rais Dkt. Samia upande wa elimu sekondari.

Amesema, tayari miundombinu ya ujenzi wa madarasa na shule unaendelea katika maeneo mbalimbali, huku akielezea kuwa kwa upande wa Shule ya Sekondari Dar es Salaam, ujenzi utaanza baada ya kukamilika kwa tathmini itayofanywa na wataalamu kutoka Chuo cha Teknolojia (DIT), kuhusu jengo hilo la ghorofa lililokaa kwa pindi cha muda mrefu bila kuisha.

“Leo hii wote kwa pamoja tunafanya kumbukizi ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kipindi chake cha miaka mitatu tangu awe madarakani, yapo mengi mazuri ambayo amefanya katika wilaya yetu, ikiwa pamoja na kutupatia fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ambapo kwa upande wa elimu sekondari ametupatia zaidi ya bilioni 24 na tayari tumeshaanza ujenzi wa shule na madarasa katika baadhi ya maeneo.

Na hata hapa kwenu tumedhamilia kujenga madarasa ya kisasa yatakayoendana na hadhi ya Jiji la Dar es Salaam, kwani kwa Jiji la Dar es Salaam kuendelea kuwa na madarasa ya chini yani msambao wakati wake umepita..hivyo naomba niwahakikishie baada ya tathmin kutoka kwa wataalamu wetu kutupatia majibu na endapo hayatakidhi, walimu mtatusamehe tutawatafutia eneo lingine na hapa tutavunja na kujenga madarasa mengine mazuri na ofisi za walimu za kisasa”, amesema Mpogolo.

Aidha amesema kuwa, anatambua changamoto ya viti na meza kuendelea kuwepo katika shule hiyo, hivyo amemtaka Afisa Elimu huyo, kutoa idadi ya viti na meza inayohitajika kwa ajili ya wanafunzi na walimu ili shule hiyo iweze kupatiwa na kudai kuwa halmashauri inazo fedha za kutosha kuweza kuwahudumia watu wake.

Nae Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mussa Ally, amesema kuwa yapo madawati 17,500 yanayotengenezwa na halmashauri hiyo yanayoendelea kupelekwa katika shule zote za Sekondari zilizo katika halmashauri hiyo.

Pia amesema kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pekee imepokea shilingi bilioni 24 , ambapo hadi sasa madarasa ya kisasa na shule zimeendelea kujengwa katika maeneo mbalimbali.

” Mhe Mkuu wa Wilaya tunashukuru sana kwa kuendelea kufanya kazi nzuri kwa wananchi wako hususani kwa wanafunzi Hawa na hata kutembelea leo katika shule hii ili kujionea miundombinu ya ujenzi na madawati yaliyotengengezwa na halmashauri, madawati tulionayo ni 17,500 na yanapelekwa katika shule zote za Sekondari zilizopo katika halmashauri yetu.

Na haya yote ni maagizo yako Mh Mkuu wa Wilaya tunakushukuru sana..kwani Nia ya halmashauri ni kuhakikisha kila mtoto anasoma akiwa katika mazingira mazuri”, amesema Ally