November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Mpogolo awafunda wazazi kata ya Vingunguti

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online,Dar

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amewataka wakazi wa Wilaya ya Ilala, kuwa na maadili mema katika malezi ya watoto wao ili kuwa na Taifa bora la baadae.

Rai hiyo imetolewa leo Septemba 14, 2024 na Mkuu huyo wa Wilaya, kwenye Mkutano wa Hadhara uliozikutanisha Kata tatu, Vingunguti, Buguruni na Mnayamani, uliofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Vingunguti ukiwa na lengo la kusikiliza na kutatua kero za wakazi wa maeneo hayo.

Mpogolo amesema malezi, ukuaji mzuri na utimamu wa akili kwa watoto uanza na wazazi hivyo ni vyema, kila mmoja akatimiza wajibu wake kwa ajili ya kupata Taifa bora la baadae.

“Niwaombe ndugu zangu wazazi hususani wa Vingunguti, Buguruni na Mnyamani kuwa makini katika malezi ya watoto, unakuta mama anacheza mziki amenyanyua Dera juu anajifunua maana yake anataka tuone nini?..alafu anacheza hivyo bila kuangalia anacheza mbele ya nani! Watu wazima watafurahia lakini tunawafundisha nini watoto wetu? hili naomba mjifunze na muwe makini nalo ili kukiokoa kizazi chetu”, amesema Mpogolo.

Pia amewataka wazazi hao, kufuatilia mienendo ya maisha ya kila siku ya watoto wao walio katika umri mdogo, ili wasijiingize kwenye masuala ya mapenzi na watu waliowazidi umri, huku akisema kuwa kufanya hivyo ni hatari kwa afya zao.

“Ukifuatilia unakuta watoto wengi wa kike ndiyo wanaoongoza kwa maambukizi ya virusi vya UKIMWI ni kwanini? Kwa sababu mabinti wengi siku hizi wanajiingiza kwenye mahusiano ya kimapenzi na watu wazima na huko ndiko wanakopatia, hivyo sisi kama wazazi tujitahidi kuwa na malezi mazuri kwa watoto wetu ili kuwaepusha na majanga hayo”, ameongeza Mpogolo.

Aidha, akijibu kero mbalimba za wananchi kutoka katika Kata hizo tatu, amesema kuwa, bado Serikali inaendelea kutatua changamoto katika maeneo mbalimbali na kupeleka miradi ya maendeleo na kuwataka wananchi kuendelea kuwa wavumilivu.