December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Mpogolo ampongeza Rais Samia kutekeleza ilani

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutekeleza yale yote yaliyoahidiwa katika ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),hususan katika Wilaya ya Ilala.

Pongezi hizo zimetolewa Agosti 2,2023 jijini Dar- es- Salaam na Mkuu wa Wilaya hiyo katika mkutano wa machinga na madereva bodaboda wa Jiji hilo uliofanyika katika uwanja vya Mnazi Mmoja, uliokuwa na lengo la kusikiliza kero zao.

Katika mkutano huo, uliohudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ambaye alikuwa Mgeni rasmi, Mpogolo amemshukuru Rais Samia kwani hadi sasa Wilaya ya Ilala imekuwa mnufaika mkubwa kupitia pochi la mama na Uviko, ambapo fedha hizo zimetumika katika ujenzi wa madarasa.

Amesema hadi sasa Ilala imepokea zaidi ya bilioni 2.1 ambazo zimetumika kumalizia madarasa,upande wa afya hadi sasa Wilaya hiyo ina vituo vya afya zaidi ya saba huku kituo kimoja kikiwa na hadhi ya ghorofa ambacho kimejengwa Mchikichini.

“Napenda kumpongeza Rasi Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri ambayo ameendelea kuzifanya hususani katika Wilaya ya Ilala kwa jografia ya Wilaya kwa Mkoa wa Dar es Salaam Ilala ndiyo Mlezi wa Wilaya zote, kwa maana yake wote tunatoka huko wilayani lakini shughuli zetu zote zinaishia hapa Ilala” amesema Mpogolo.

Aidha amesema kuwa, kati ya mikoa yenye changamoto ya kiuendeshwaji ni Dar es Salaam kutokana na kuwa ndiyo Mkoa wenye idadi kubwa ya watu ambao zaidi ya milioni 5.3, huku akidai kuwa kati ya watu hao wenye changamoto nyingi zaidi ni machinga na madereva bodaboda.

Amesema, kwa kuzingatia hilo Serikali itahakikisha inajenga masoko makubwa manne, ambapo kati ya hayo soko la kwanza kujengwa litakuwa la Ilala kwa madai kuwa ndilo lenye wafanyabiashara zaidi ya 1200.

Ametaja masoko mengine ambayo yatajengwa baada ya soko la Ilala, ni pamoja na soko la Mchikichini, Gongo la Mboto na Chanika.

Aidha Mpogolo amesema kuwa, tayari kimeandaliwa kikosi maalumu kitakacho hakikisha kinaangalia usalama wa madereva bodaboda na machinga ili wasiweze kusumbuliwa bila sababu na kudai kuwa, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa kushirikiana na Ofisi za Jiji watahakikisha wanaandaa maeneo maalumu na yaliyo na muonekano mzuri kwa ajili ya watu hao.