December 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Mpogolo aitaka NACONGO kuwa wazalendo kwa Taifa


Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameyataka mashirika yasiyo ya kiserikali (NACONGO), kuwa wazalendo na kutokubali kutumika vibaya kwa lengo la kuligawa Taifa.

Mpogolo amesema hayo jana Agosti 19, 2024, Jijini Dar es Salaam, wakati akifungua mkutano ulioyakutanisha mashirika hayo, ambao ni wadau wakubwa wa Serikali, huku akiyashukuru kwa kazi kubwa ambayo yamekuwa yakifanya katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika sekta ya elimu, uchumi na masuala ya kijamii kwa ujumla hususani katika Wilaya ya Ilala.

“Napenda kuwapongeza sana kwani mashirika yasiyo ya Serikali yamekuwa yakifanya kazi kubwa katika kuunga mkono juhudi za Serikali hususani kwenye Wilaya yetu ya Ilala katika sekta mbalimbali, hivyo ombi langu kwenu nikiwa kama Mwenyekiti na mlezi wenu nawaomba muwe wazalendo kwa Taifa letu na kutokubali kutumika na watu au mataifa yasiyolitakia mema Taifa letu kwani kufanya hivyo kinaweza leta machafuko nchini jambo ambalo si jema”, amesema Mpogolo.

Aidha, DC Mpogolo amesema, kwa kutambua mchango wa mashirika hayo, Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano na kuweka utaratibu wa kukutana nayo ili kuelezea mafanikio yaliyofanywa na Serikali ndani ya kipindi Cha miaka mitatu ya Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Ambapo kati ya mafanikio aliyotaja ni pamoja na Wilaya ya Ilala kupokea kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo inayoendelea kufanyika katika Wilaya hiyo.