November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Mpogolo afungua mafunzo ya mabadiliko ya mtazamo katika usimamizi miradi

-Wakuu wa Idara na Watendaji kukiona wasipokamilisha miradi kwa wakati

Na Agnes Alcardo, TimesMajira Online

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ametoa angalizo kwa wakuu wa Idara na watendaji katika Wilaya hiyo, watakaoshindwa kukamilisha miradi kwa wakati na viwango vinavyohitajika kuwajibishwa.

Mpogolo ameyasema hayo leo Jijini Dar es Salaam, wakati akifungua mafunzo ya mabadiliko ya mtazamo katika usimamizi wa miradi ya Wilaya ya Ilala, kwa wakuu na viongozi mbalimbali wa Idara katika wilaya hiyo, yaliyoanza leo na kutarajiwa kumalizika kesho.

Mpogolo amesema, mafunzo hayo ni matokeo ya mwaka mmoja baada ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo na kubaini uwepo wa mapungufu, ambapo amesema kuwa, kupitia mafunzo hayo hivi sasa wakuu wa idara na watendaji watakuwa na uwezo wa kuisimia kikamilifu na watakaofanya tofauti watachukuliwa hatua.

” Mafunzo haya ni matokeo ya mwaka mmoja baada ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo na kubaini mapungufu katika miradi hiyo kwa waandisi, watu wa manunuzi, wachumi nk hivyo natumai kupitia mafunzo haya miradi itakamilika kwa viwango vinavyohitajika na wakati ikiwa pamoja na utolewaji wa taarifa kwa wakati kwa upande wa wachumi, endapo kutakuwa na mtu ambaye atafanya tofauti baada ya mafunzo haya basi ni lazima atawajibishwa.amesema mpogolo.

Amesema ni vyema watumishi, wakuu wa idara, kamati za ununuzi, waandisi na kamati za ujenzi kubadilika katika usimamizi wa Miradi ya maendeleo ili ilete tija kwa wananchi baada ya mafunzo hayo yaliyotolewa na Mkuu wa Chuo Cha Usimamizi wa Miradi, Lwitiko Mwalukasa.

Aidha ameongeza kuwa, Ilala ndiyo Halmashauri inayoongoza kwa mapato kuliko Halmashauri zote, hivyo ni vyema hata miradi yake ikawa yenye kiwango cha kuvutia zaidi, huku akiwataka watendaji wa Kata kutoa taarifa sehemu husika pindi wanapoona kusuasua kwa miradi.

Kwa upande wake, Meya wa Jiji la Dar es salaam, Omary KumbilaMoto, amemshukuru Mkuu wa Wilaya hiyo kwa kuwapa fursa ya mafunzo hayo, ambayo anaamini yataleta Mabadiliko katika miradi mingi ikiwa pamoja na kukamilika kwa wakati.

Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jomaary Satura, amesema kupitia mafunzo hayo atahakikisha anaongeza nguvu katika Mapinduzi ya usimamizi kamilifu wa miradi na kuhakikisha inajulikana tarehe ya kuanza na kukamilika kwake.

Mafunzo hayo yameshirikisha wakuu wa idara, maafisa tarafa, maafisa ununuzi, waandisi, wachumi, wenyeviti wa kamati za kudumu, maafisa elimu kata, watendaji kata na mameneja kanda.