January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Mpogolo aelezea mafanikio ya Ilala miaka 3 ya Rais Samia

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online.Dar

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, ameielezea miaka mitatu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,imekuwa ya mfano katika kuchochea maendeleo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo siasa, uchumi na jamii kwa ujumla.

Mpogolo, ameyasema hayo Machi 16, 2024, katika mafunzo ya ulipaji kodi yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA, kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) pamoja na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), yaliyotolewa kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Mpogolo amesema kuwa katika kipindi hicho Wilaya ya Ilala imeendelea kunufaika kwa kupokea fedha kutoka Serikali kuu, ambazo zimeendelea kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilayani humo.

“Ninapoelezea mafanikio ya miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhi Hassan, katika Wilaya ya Ilala, tumefanya mambo mengi ya kimaendeleo katika sekta mbalimbali, ikiwa pamoja na kupokea zaidi ya bilioni 4 katika miradi ya barabara na mradi wa DMDP awamu ya pili, utakuwa na ujenzi wa barabara wa kilometa 20 pamoja na mifereji na masoko yenye hadhi ya kimataifa,”.

Upande wa elimu ya msingi, imefanikiwa kujenga madarasa ya kisasa kwa kila shule huku kwa upande wa elimu ya sekondari imejenga madarasa ya mtindo wa ghorofa katika shule zote za Kata kati ya hizo zipo zilizokamilika na nyingine zikiwa katika hatua za mwisho lengo ni kuendana na kasi ya ongezeko la wanafunzi.

Pia, ametaja miradi mingine inayoendelea kufanya vizuri ni pamoja na ya sekta ya afya na maji, huku akitaja kuwepo kwa ongezeko la fedha za mikopo katika halmashauri hiyo.

Aidha ametoa shukrani kwa wawezeshaji wa mafunzo hayo na kudai kuyafanyia kazi, huku akiwasihi wanachama wa CCM kuwa mfano na kuweka uzalendo mbele kwa kutoa na kudai risiti kwa maendeleo ya Taifa.