November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Mkanachi awataka wafugaji kuheshimu sheria na kanuni za uhifadhi

Na Said Njuki,TimesMajira Online,Kondoa

SERIKALI wilayani Kondoa,Mkoa wa Dodoma,imezitaka jamii na wahifadhi kwa pamoja kuheshimu sheria na kanuni za uhifadhi ili kuepuka migogoro isiyo na lazima.

Rai hiyo imetolea na Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Khamisi Mkanachi wakati wa mahojiano maalumu na gazeti juzi, huku akibainisha sababu kuu za migogoro hiyo katika mapori ya akiba ya Mkungunero na Swagaswaga yaliyopo wilayani hapa.

Katika kukomesha hali hiyo, Mkuu huyo alisema kumekuwa na migogoro ya muda mrefu katika hifadhi hizo, moja ya sababu upanuzi wa mipaka ya hifadhi hizo, sanjari na kudorora kwa mahusiano kati ya wakulima na wafugaji wanaopakana na hifadhi hizo kwa upande moja na wahifadhi kwa upande mwingine jambo ambalo haliwezi kuvumilika.

“Tunahifadhi hizo mbili (mapori ya akiba) wilayani hapa na sisi tunaziona ni ‘tunu’ toka kwa Mwenyezi Mungu…tumependelewa Sana, tunachopaswa kukifanya ni kuzihifadhi bila kusababisha migogoro isiyo ya lazima nawahakikishia serikali haitakubali hilo kwa faida ya jamii na taifa kwa ujumla” alisema Mkanachi.

Alisema changamoto kuu ni mbili katika hifadhi hiyo, kwa Mkungunero alisema tatizo lilianza mwaka 2006 baada ya serikali kuhakiki mipaka yake ya awali ya mwaka 1995 na kuongeza hadi maeneo ya jamii jambo lililozusha mtafaruku mkubwa hadi leo.

“Inasadikika mipaka ya Pori hilo iliongezeka mwaka 2006 baada ya kufanya uhakiki, hata hivyo inadaiwa jamii haikushirikishwa kama ikivyokuwa kwenye zoezi kama hilo mwaka 1995 hapo ndipo palipoanza chokochoko kwani unapoongeza eneo la uhifadhi, maana yake unaopunguza maeneo ya makazi, kilimo na ufugaji” aliongeza Mkuu huyo.

Alisisitiza kwamba muhimu katika hili ni kusimama katika sheria za uhifadhi, wahifadhi watambue wafugaji na wakulima ni wahifadhi pia na wafugaji wajue wao ni sehemu ya wahifadhi, tofauti na hilo migogoro utaendelea na madhara zaidi yataendelea kutokea.

“Hifadhi na uhifadhi ni jambo muhimu lazima sote kama watanzania tushiriki kikamilifu kuhakikisha hifadhi zetu zinakuwa endelevu…lakini kwa upande mwingine pia wafugaji na ufugaji, wakulima na ukulima wao ni muhimu katika kukuza pato la taifa na kuimarisha lishe kwa jamii zetu, hivyo ni wajibu wetu kuwalinda”

Alisema serikali ilishasikia kilio chao, kaunda kamati mbalimbali na kufanya uchunguzi wa kina juu ya mkanganyiko huo, hivyo anaamini kazi hiyo ilishakamilika kilichobaki ni tamko la serikali hiyo kwa mujibu wa taratibu, kanuni na sheria.

Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Khamisi Mkanachi

Aliomba viongozi wa hifadhi hizo kutekeleza sera ya ujirani mwema ambapo hutakiwa kushiriki katika maendeleo ya huduma za jamii kwa kuchangia ama kushiriki maeneo yanayopakana na hifadhi hizo kwani licha ya kusukuma maendeleo mbele pia huimarisha mahusiano mazuri baina yao.

“Angalia lile ongezeko la hifadhi liliwakuta watu wengine tayari wanayo makazi yao kule, wakilima pia wakifuga, serikali kwa kutambua hilo akiamuru wasiondolewe kwa masharti ya kutii sheria hadi serikali itakapotoa maelekezo mengine jambo linalosubiriwa kwa hamu kubwa” alisema.

Kwa muda mrefu kumekuwa na matukio kadha wa kadha ya migogoro katika mapori hayo mawili ya akiba, Pori la Mkungunero na Swagaswaga ambapo idadi kadhaa ya wafugaji na wakulima wamekumbana na mkono washeria kwa kuingia au kuongiza mifugo hifadhini.

Kwa upande mwingine hali hiyo imekuwa ikizorotesha mahusiano baina yao jambo linalosababisha uadui kuwa mkubwa baina ya pande hizo mbili.

Mwisho