Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya
MKUU wa Wilaya ya Mbeya, Solomon Itunda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, hususan katika kipindi cha siku 100 za uongozi wake kwa awamu ya pili.
Akizungumza Januari 3, 2026 katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya pili kilichojadili taarifa ya mwaka wa fedha 2025/2026, Itunda amesema Serikali imeongeza fedha za mradi wa kimkakati wa barabara kutoka Igawa hadi Tunduma kutoka shilingi bilioni 128 za awali hadi bilioni 185.
“Mpaka sasa fedha hizo zimeshaingia, na katika Jimbo la Uyole tayari wameshaanza kutandaza lami. Kazi kubwa imefanyika ndani ya siku 100 za Rais Dkt. Samia, na miradi mingi imetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini,” amesema Itunda.
Ameongeza kuwa kuna mradi mkubwa wa maji unaolenga kumaliza changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Mji wa Mbalizi na maeneo ya Mbeya mjini, unaotumia chanzo cha Mto Kiwira kilichopo Wilayani Rungwe.

“Kwa niaba ya wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, namshukuru Rais kwa namna anavyoendelea kuijali wilaya yetu. Tumepata upendeleo mkubwa na hatuna budi kumshukuru,” amesema.
Aidha, Itunda ameutaka uongozi wa Halmashauri kuendelea kushirikiana na madiwani katika kusimamia ukusanyaji wa mapato, akibainisha kuwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo unategemea upatikanaji wa fedha za ndani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Erica Yegella, amemuhakikishia Mkuu wa Wilaya kuwa wataendelea kusimamia ipasavyo miradi yote ya maendeleo bila vikwazo.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Aida Haule ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Utengule Usongwe, amesema watahakikisha fedha za maendeleo zilizotolewa zinafuatiliwa kwa karibu katika miradi yote ikiwemo ule wa Mji Mdogo wa Mbalizi.
Bakari Juma, mkazi wa Kata ya Utengule Usongwe, amesema mradi wa kimkakati wa barabara ya njia nne umeleta tija kubwa, ukisaidia kupunguza msongamano wa magari, ajali na kuongeza usalama kwa watembea kwa miguu.

More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama