January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC.Masala: Ilemela tunaendelea kutatua changamoto upungufu wa madarasa

Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza

Wilaya ya Ilemela inaendelea kupambana ili kutatua changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa unaosababishwa na idadi kubwa ya wanafunzi shuleni inayotokana na mwitikio wa wazazi kuwapeleka watoto wao shule.

Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala,Februari 28, 2024,wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Buswelu katika kikao chake cha kwanza cha ziara ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Wilaya hiyo kilichofanyika kwenye ofisi ya Mtendaji wa Kata hiyo.

“Hali hiyo inasababisha upungufu wa vyumba vya madarasa kwa baadhi ya shule ikiwemo ya Buswelu,ukienda sasa hivi kuna watoto wanakaa chini, tunaendelea kupambana ili kuondokana changamoto hiyo ndio maana tunaongeza shule mpya,tumeisha jenga nyingine Busenga,Bujingwa huko kote tunajenga miundombinu ya shule ili tupunguze watoto hawa tuwahamishie kule,”.

Masala ameeleza kuwa elimu ni kipaumbele chao hivyo wanaanza utengenezaji wa madawati awamu ya pili kwa ajili ya wanafunzi ambayo watayapeleka kwenye shule zote ndani ya mwaka huu wa fedha ambapo utekelezaji utaanza Machi mwaka huu.

Kwa upande wake Ofisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Mwalimu Sylvester Mlimi, ameeleza kuwa ili mwanafunzi afanye vizuri kitaaluma lazima ahakikishiwe usalama wa afya yake hususani hupatikanaji wa chakula na kwa sasa wanasisitiza na wameongeza muda ili watoto wasome kwa muda unaotosha katika Halmashauri yao shule nyingi wanafunzi wanatoka saa 11 jioni.

“Huu ni mpango wa kuhakisha taaluma yetu inapanda hivyo tunaomba wananchi na wazazi mtusaidie huduma ya chakula,kila mzazi amfuatilie mtoto wake ajue anafanya nini darasani,mtoto akifika nyumbani mkague daftari lake siku hiyo ameandika kama hakuandika muulize kwanini hakuandika kwa kufanya hivyo mtatusaidia watoto waweze kufanya vizuri,”ameeleza Mwalimu Mlimi na kuongeza:

“Pia wazazi wahakikishe hakuna utoro kwa watoto wao,unapoondoka nyumbani jiridhishe mtoto ameenda shuleni siyo kwa kumuona amevaa sare lakini pia upate muda wa kwenda shuleni kujiridhisha kama mtoto anafika shule,
tumeshuhudia watoto wetu hawafiki shuleni,”.

Pia amesema mpango mwingine wa muda mfupi ni kuhakikisha shule zinashindana mara kwa mara kwa kufanya mazoezi na mitihani ya mara kwa mara ili kufanya wanafunzi kuwa imara.

“Tunakuwa na vikao vya mara kwa mara tunawashirikisha wazazi na pale inapobidi wanachangia kwa maana ya kuleta rimu,kupitia kibali maalumu cha Mkuu wa Wilaya ili watoto wafanye mazoezi na mitihani ya mara kwa mara,”.

Aidha ameeleza kuwa mpango wa muda mrefu ni kuhakikisha wanajenga shule karibu ili kuwapunguzia kupunguza umbali kwa baadhi ya wanafunzi wanatoka maeneo yalio mbali na shule.

“Maelekezo ya serikali ya sasa hivi ni kuandaa mpango wa kila kijiji au mtaa kuwa na shule hivyo wananchi tunawaomba tunapo hitaji kutumia maeneo yenu kwa suala la elimu mtupe ushirikiano kwa sababu shule za Kata zimezidiwa kwa wingi na umbali umekuwa changamoto huku usafiri kwa wanafunzi ni shida,”ameeleza Mlimi na kuongeza:

“Pia kila shule kuwa na maabara tatu hivyo wanafunzi kusoma kwa vitendo ndio maana tunaimarisha mitihani kwa vitendo na tulikuwa na changamoto ya Walimu wa Sayansi tumeisha peleka maombi maalumu kwa serikali,”.

Naye mmoja wa wakazi wa Kata ya Buswelu Charles Vedastus, ameiomba serikali kupitia Mkuu huyo wa Wilaya kujenga shule ya bweni ili kusaidia watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu pamoja na kuzuia mimba za utotoni ambazo zinaweza kujitokeza.

Hata hivyo Mkuu wa Wilaya Hassan Masala akijibu ombi la mwananchi huyo ameeleza kuwa tayari wameisha anza kujenga mabweni kwa baadhi ya shule wilayani humo ikiwemo sekondari ya Igogwe,Buswelu na Kilimani.

“Na kwa sasa tunatoa maeneo ambayo mipango yetu yote itajielekeza katika kujenga shule za bweni zaidi ili kuondoa changamoto ya watoto wetu kukatishwa masomo,”.