Judith Ferdinand, Timesmajira Online, Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Hassan Masala ameiagiza Mamlaka ya MajiSafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mwanza (MWAUWASA) kuhakikisha inaweka utaratibu rafiki wa kutoa huduma ya kusambaza maji ili kuondoa usumbufu usio wa lazima kwa wananchi.
Kauli hiyo ameitoa wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi wa Kata ya Mecco ilioenda sambamba na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa ndani ya kata hiyo.
Masala amesema kuwa ni wajibu wa MWAUWASA kuhakikisha inaweka utaratibu mzuri wa kusambaza maji kwani Serikali inafanya jitihada kubwa katika kuondoa kero ya uhaba wa maji ambayo imekuwa ya muda mrefu sasa.
Akifafanua kuhusu kero ya maji Masala amesema kuwa kwa Wilaya ya Ilemela pekee imeshapokea magari ya kutosha ya mabomba ya kusambazia maji katika maeneo ambayo yanakabiliwa na upungufu wa maji kwa kiasi kikubwa.
Pia amesema Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa vyanzo vipya vya maji ikiwemo cha Butimba na matarajio ya kuanzisha chanzo kipya cha Kabangaja ili kusaidia upataikanaji wa maji ya uhakika kwa wananchi wa Ilemela na Mkoa wa Mwanza kwa ujumla wake.
Kwa upande wake Meneja Msaidizi wa Idara ya maji MWAUWASA Kanda ya Nyakato Juma Saidi mbali na kukiri kupokea fedha nyingi kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya kuboresha sekta ya maji amesema kuwa mamlaka hiyo inaendelea na taratibu za kusambaza maji kwa wananchi kulingana na utaratibu uliowekwa ili kuhakikisha kila eneo lenye changamoto linapatiwa ufumbuzi pamoja na kuwaomba wananchi kuwa wavumilivu wakati mamlaka hiyo ikiendelea na kazi zake
Diwani wa Kata ya Mecco Godlisten Kisanga amemshukuru mkuu huyo wa wilaya ya Ilemela kwa jitihada zake katika kutatua kero za wananchi sanjari na kuwaomba wananchi kuungana na Serikali katika kufanikisha shughuli za kila siku za maendeleo
More Stories
AZAKI yawasilisha mapendekezo yao kwa Serikali katika kuboresha Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050
CP.Wakilyamba :Uvamizi maeneo ya hifadhi ya taifa katavi haukubaliki
Watu wawili wanaodhaniwa majambazi wapigwa risasi na Polisi