November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC. Makilagi atoa elimu ya umuhimu wa sensa na kuhimiza wananchi kushiriki

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Agosti 23, mwaka 2022 taifa linatarajia kufanya sensa ya watu na makazi,hivyo wananchi wa Wilaya ya Nyamagana wamehimizwa kila mtu kwa nafasi yake kushiriki zoezi hilo kwa kutoa taarifa sahihi.

Akizungumza katika mkutano wa wadau kwa ajili ya kuhamasisha sensa ya watu na makazi kwa Wilaya ya Nyamagana, Mwenyekiti wa kamati ya sensa Wilaya hiyo,Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi, amesema katika kuhakikisha Agosti 23 kila mtu anahesabiwa walianda mpango kazi.

Makilagi ameeleza katika mambo walioyapa kipaumbele ni kutoa elimu kwa wananchi wa Nyamagana ili kufikia Julai 16 mwaka huu kila mwananchi wilayani humo awe ameishapata uelewa juu ya sensa.

Sensa inakwenda kusaidia mipango ya taifa na ustawi wa taifa itafanyika nchi nzima na kuhusisha watu wote watakao lala ndani ya mipaka ya Tanzania huku taarifa zote zitakazotolewa ni za siri na zitatolewa katika masuala ya kitaaluma tu.

Hivyo Makilagi amewataka wananchi wasiwe na hofu kwani lengo la zoezi hilo ni kupata taarifa sahihi zitakazowezesha serikali na wadau wengine kupanga mipango ya maendeleo ya watu na taifa katika sekta mbalimbali.

“Zoezi la sensa ya watu na makazi kwa taifa na Wilaya ya Nyamagana ni zoezi ambalo kila mmoja wetu na kwa kila nafasi yake ni lazima ashiriki na kutimiza wajibu wetu kwa kutoa taarifa sahihi ili kuhakikisha adhima ya serikali ya kupata takwimu sahihi kwa upangaji wa mipango ya maendeleo ya taifa letu inaweza kufikiwa,”ameeleza Makilagi.

Kwa upande wake Mratibu wa sensa Wilaya ya Nyamagana Ruhinda Constantine, ameeleza kuwa sensa ya mwaka huu itafanyika kwa kutumia teknolojia ya kisasa itahusisha mazoezi matatu muhimu ambayo ni sensa ya majengo,anwani za makazi na zoezi la kuhesabu watu.

Constantine ameeleza kuwa faida za sensa ni huiwezesha serikali kupanga bajeti inayokudhi matakwa ya wananchi na maeneo wanayoishi kwa kuzingatia umri,jinsia,ajira,elimu zao na maisha ya wananchi kiujumla.

Ameeleza kuwa takwimu zinazotokana na sensa huwezesha mipango ya elimu yenye kuzingatia ushahidi wa takwimu kuhusu maamuzi ya wapi shule ijengwe kutokana na wingi wa Watoto wenye umri wa kwenda shule.

Idadi ya madarasa,matundu ya vyoo na miundombinu ya huduma ya usafi shuleni kulinganavna wingi wa wanafunzi,idadi ya walimu unaozingatia uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi pia mahitaji ya vifaa vya kufundishia.

Pia ameeleza kuwa,takwimu zinazotokana na sensa huwezesha mipango ya afya yenye kuzingatia ushahidi wa takwimu kuhusu maamuzi ya wapi kituo cha afya lijengwe kutokana na wingi wa watu.

Sanjari na hayo ameeleza kuwa athari za kutofanya sensa ni pamoja na serikali kupanga bajeti ambayo haiaksi mahitaji halisi ya wananchi.

“Hii huchelewesha maendeleo,huondoa amani kwa wananchi na kichocheo cha kuongeza umaskini,hivyo wananchi wote wajitokeze katika zoezi hili na kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa watakao pita katika nyumba zao na wajiandae kuhesabiwa,”ameeleza Constantine.

Mmoja wa washiriki wa mkutano huo Mwenyekiti wa Soko Kuu jijini Mwanza Ahmed Nchola,amewahimiza wananchi wenzake kujiandaa kuhesabiwa katika zoezi hilo kwa manufaa ya taifa na ili serikali ifikie malengo ya kuleta maendeleo kwa wananchi wake.

“Wananchi wenzangu zoezi hili ni muhimu sana na taifa lolote ambalo linamaendeleo lazima sensa ilifanyika hivyo mimi nitakuwa mstari wa mbele kuhamasisha watu waweze kushiriki katika zoezi hili,”amesema Nchola.

Mkutano huo ambao ilifanyika katika chuo cha ualimu Butimba kilishirikisha watu zaidi ya 700 kutoka makundi mbalimbali wilayani humo ikiwemo watu wenye ulemavu,bodaboda, wafanyabiashara, viongozi wa dini,wanasiasa na wengineo.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi akizungumza katika mkutano wa wadau kwa ajili ya kuhamasisha sensa ya watu na makazi kwa Wilaya ya Nyamagana, uliofanyika katika chuo cha ualimu Butimba jijini Mwanza.(Picha na Judith Ferdinand)
Mratibu wa sensa Wilaya ya Nyamagana Ruhinda Constantine akizungumza katika mkutano wa wadau kwa ajili ya kuhamasisha sensa ya watu na makazi kwa Wilaya ya Nyamagana, uliofanyika katika chuo cha ualimu Butimba jijini Mwanza.(Picha na Judith Ferdinand)
Baadhi ya watu waliohudhuria katika mkutano wa wadau kwa ajili ya kuhamasisha sensa ya watu na makazi kwa Wilaya ya Nyamagana, uliofanyika katika chuo cha ualimu Butimba jijini Mwanza.(Picha na Judith Ferdinand)