January 9, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dc. Mahawe ataka wananchi Ihanda kuwa na subira.

Na Moses Ng’wat,Timesmajira Online,Mbozi

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Esther Mahawe amewataka wananchi wa Kijiji Cha Iboya, Kata ya Ihanda, wilayani humo kuwa watulivu wakati serikali inaendelea na taratibu kwa ajili ya kulipa fidia baada ya kuachia maeneo yao ili kupisha ujenzi wa mradi wa kituo cha ukaguzi wa pamoja wa magari makubwa ya mizigo yaendayo nje ya nchi.

Mahawe amesema hayo mwishoni mwa wiki alipokutana na wananchi wa eneo hilo kusikiliza kero yao

“Nimekuja kuwasikiliza,fedha inatafutwa na Serikali na kila mtu atapata haki yake,mmnaomba leo iwe Siku ya mwisho kutoa elimu, ifike mahali tuelewane,” amesema DC Mahawe na kuongeza kuwa

“Ndugu zangu hii ni Serikali haichezewi, hakuna aliyejuu ya sheria,mlipewa vizuri elimu, watu wanaitisha vikao tumekuja kutoa elimu kwa mara ya mwisho,ninyi sio pekeyenu mnadai fidia
hatutakubali kuinyima Wilaya amani,”.

Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe, Mhandisi Salvan H. Mloka amesema kuwa “Mradi huu upo na mpaka sasa kuna wataalamu wameshafika katika Wilaya yetu,tutaanza kwa maana hiyo ni kitu ambacho kipo na fedha itakapopatikana mtaziona tu,”.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, George Musyani ameeleza kuwa Wananchi wa Ihanda wana wajibu wa kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea mradi huo.

“Kupitia mradi huu wana Ihada wana wajibu kumshukuru usiku na mchana Rais sasa mivutano hii inakuwa sio sawa,mradi huu utachochea ukuaji wa Wilaya na ukuaji wa maendeleo kwa ujumla,wanaIhanda kuweni wa moja,inapokuja miradi ndo maendeleo yanakuja na mradi huu utakuza pato la halmashauri,” ameeleza Mwenyekiti huyo na kuongeza kuwa

“Tufuate itifaki za uongozi kama una kero tushirikishane kwa kufuata utaratibu , tuna kiu sana na mradi huu,”.