Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
MKUU wa Wilaya ya Mkalama, Mhe. Moses Machali, amekipongeza kwa dhati Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu nchini, akisisitiza kuwa chuo hicho kina nafasi ya kipekee katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Taifa.
Akizungumza mara baada ya kutembelea banda la UDSM katika Maonesho ya Wakulima (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma, Mhe. Machali alisema amevutiwa na teknolojia mbalimbali zilizobuniwa na wanafunzi na watafiti wa chuo hicho, zikiwemo zinazolenga sekta za kilimo, ufugaji na urembo.
“Tumeshuhudia mabinti wadogo wakitengeneza bidhaa zenye thamani kama mafuta ya asili yanayosaidia kuondoa makunyanzi. Hii ni ishara kwamba UDSM si tu chuo cha kufundisha nadharia, bali kinakuza ubunifu wa vitendo unaogusa maisha ya kila siku ya Mtanzania,” alisema DC Machali.
Aidha, alielezea kuvutiwa na teknolojia ya kisasa katika sekta ya ufugaji wa samaki, hususan mashine ya kukamata vifaranga bila kutumia mikono, ambayo kwa mujibu wa wataalamu, inapunguza vifo vya vifaranga kwa zaidi ya asilimia 25 ikilinganishwa na mbinu za kawaida.
“Ni teknolojia rafiki kwa maisha ya samaki. Nawahimiza wafugaji na wazalishaji wa vifaranga nchini kutembelea banda la UDSM ili kujifunza teknolojia hizi zitakazoboresha uzalishaji na kupunguza hasara,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Mhe. Machali alisifu jitihada za kidijitali zinazofanywa na chuo hicho kupitia programu mahususi za simu (mobile apps) zinazowaunganisha wakulima moja kwa moja na watoa huduma za kilimo.
“Kupitia apps hizi, mkulima anaweza kupata huduma zote muhimu akiwa kijijini kwake. Hii inapunguza gharama na muda wa kusafiri kufuata huduma za maafisa ugani,” alibainisha.
Mhe. Machali aliipongeza Ndaki ya Masuala ya Kilimo na Teknolojia ya UDSM kwa jitihada na mchango wake mkubwa kwa maendeleo ya Taifa, akisisitiza kuwa uwepo wao katika maonesho ya Nanenane unatoa picha halisi ya namna taasisi za elimu ya juu zinavyoweza kuchochea mabadiliko chanya katika jamii.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi