Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto
MKUU wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Zephania Sumaye amewataka madiwani kwenda kuwahamasisha wanawake wenye uwezo kugombea uongozi kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kujitokeza.
Amesema anaamini wanawake wakiwa wengi kwenye uongozi wa vijiji, mitaa na vitongozi, kesi za kuuzwa ardhi mara tatu tatu zitapungua, sababu wanawake ni waaminifu sana kwenye uongozi kuliko wanaume, hivyo watapunguza migogoro ya ardhi.
Ameyasema hayo Septemba 11, 2024 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, na kuongeza kuwa wanaume wasiwazuie wanawake kugombea uongozi kwa imani za kidini, kwani hata wanawake wana haki kuwa viongozi.
“Hapa kwenye Baraza wanawake wamejaa, lakini kule kwenye Serikali za Mitaa hakuna hata mmoja, kwa hiyo muende mkawahamasishe wanawake wengine,masuala ya kuathiriwa na itikadi za dini tuyaache twendeni tukagombee Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Naamini wanawake wanapokuwa viongozi hata ile mihuri ya kuuza ardhi feki inapungua,akina baba msinipige mawe, sasa huo ndiyo ukweli. Ile mihuri feki ya kuuza ardhi mara tatu Mwenyekiti akisimamia, wanawake wakiwepo hizo kesi sio nyingi, hivyo tuwahamasishe na tunaamini uaminifu wenu ni mkubwa sana kuliko sisi hivyo nendeni mkawahamasishe wanawake wenye uwezo, sio wasio na uwezo, bali wenye uwezo wachukue fomu na wagombee uongozi wa Serikali za Mitaa” amesema Sumaye.
Wakati huo huo Sumaye amewatahadharisha wananchi wa Wilaya ya Lushoto kutokana na nchi jirani kuzingirwa na ugonjwa wa Homa ya Nyani kitaalamu Mpox, hivyo Lushoto ikiwa ni moja ya wilaya zinazopakana na nchi jirani hizo, wazingatie suala la usafi kwani kama ilivyokuwa kwenye ugonjwa wa UVIKO 19, wananchi wanatakiwa kuwa wasafi kwa kunawa mikono.
Hivyo, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Ikupa Mwasyoge akishirikiana na Ofisa Afya na Ofisa Mazingira, kuhakikisha kila eneo la taasisi na shughuli za umma kama stendi na kwenye masoko kunakuwa na ndoo za kunawia mikono, hiyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na ugonjwa huo.
“Kwa tafiti zilizofanyika, usafi wa kunawa mikono unapunguza magonjwa ya kuambukiza kwa asilimia 30, hivyo Mwenyekiti mbele ya Baraza lako niwatake, sana sana Mkurugenzi, kuhakikisha kwamba katika maeneo ya taasisi za Serikali pamoja na maeneo ya masoko na stendi kunawekwa vitakasa mikono ili wananchi wawe na desturi za kunawa mikono.
“Ukienda pale stendi utakuta watu wanauza kuku, wanauza matunda, lakini utakuta ndoo za maji zipo kule nyuma yao, na sio wote wanazo na ndoo hizo ni chafu kuliko mikono yetu, kwa hiyo hapo ni tatizo.
“Kwa hiyo Mkurugenzi kupitia Wakuu wa Idara, Afisa Afya, Afisa Mazingira ambao wapo hapa, nataka mkahakikishe pale stendi panakuwa pasafi,si tu vitakasa mikono, lakini hata mitaro na mazingira tunaweka Lushoto yetu safi” amesema Sumaye.
Sumaye alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji, Mwasyoge kwa kujenga Kituo cha Utalii, kwani sio halmashauri ama wilaya zote wana kituo kama hicho,lakini pia amempongeza Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Mathew Mbaruku, kwani kuna wakati alitumia fedha zake za mfukoni kuhakikisha kituo hicho kinakamilika.
Sumaye amesema wapo kwenye maandalizi ya Tamasha la Usambara Tourism Festival. Tamasha hilo lilikuwa lifanyike Septemba, mwaka huu, lakini wamelisogeza mbele hadi Novemba, mwaka huu, na malengo ya kusogeza mbele ni kuona tamasha hilo linaleta tija.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Hatibu Ulanga, ambaye ameshinda nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo, huku akipigiwa kura za ndiyo na madiwani wote 44, aliwataka wananchi hasa wanaoishi kwenye kata yake ambao hawako mbali na nchi ya Kenya, waweze kufuata ushauri wa maofisa wa afya ili kujilinda na ugonjwa wa Mpox.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best