January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Lushoto: Mtendaji Kata kupimwa kwa ukusanyaji mapato

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto

MKUU wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Japhari Kubecha ametaka kipimo cha Ofisa Mtendaji Kata kiwe ni ukusanyaji mapato kwenye kata yake na kama atashindwa, aondolewe kwenye nafasi hiyo na kupelekwa kupanga mafaili masjala ya halmashauri.

Hivyo amemuomba Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Ikupa Mwasyoge pamoja na Madiwani kuwa wakali kwa Watendaji hao waweze kusimamia na kukusanya mapato vizuri, ikibidi waombe Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Ofisa Biashara wa Halmashauri kwenda kutoa elimu kwa watendaji hao jinsi ya kukusanya mapato.

Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Japhari Kubecha akizungumza kwenye Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto. Wengine ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Mathew Mbaruku (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Ikupa Mwasyoge (kulia).

Ameyasema hayo Mei 24, 2024 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto lililojadili taarifa za kata ikiwemo utekelezaji wa miradi ya maendeleo na ukusanyaji mapato kwenye kila kata ambapo Watendaji wa Kata ni Wajumbe wa kikao hicho huku halmashauri hiyo ikiwa na kata 33.

“Mapato bado yapo chini katika robo ya tatu, inaonesha kuna mahali mambo hayajakaa sawa, DED tunaomba uwapime watendaji kutokana na ukusanyaji wao wa mapato kama atashindwa kufikia malengo aondolewe na kurudishwa masjala na badala yake atafutwe mtu ambaye atatuwezesha kukusanya mapato,”amesema Kubecha na kuongeza

“Madiwani mkiona tunawang’oa watendaji wenu mtatuwia radhi maana tunataka mapato sababu ndiyo kitu muhimu katika kufanikisha shughuli za maendeleo, ikibidi, muwaombe TRA na Ofisa Biashara wa Halmashauri kwenda kutoa elimu ya ukusanyaji kodi,”.

Kubecha amesema mwaka huu ni wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo ametaka wachaguliwe viongozi watakaoweza kusaidia kusukuma maendeleo ya wananchi.

“Tunataka tupate wenyeviti wa kuweza kusukuma maendeleo ya wananchi mbele ikiwemo kukusanya mapato,hatutaki wenyeviti wauza viwanja na kusabsbisha migogoro,”amesema Kubecha.

Akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari mara baada ya kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ikupa Mwasyoge,amesema wamechukua hatua kwa Watendaji wa Kata ambao wameshindwa kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato kwa kuwaandikia barua ya kuwataka wajieleze sababu ya kushindwa kukusanya mapato.

Mwasyoge amesema kama halmashauri, wanafanya jitihada za kufikia malengo ya ukusanyaji mapato, kwani kwa robo ya tatu kwa mwaka wa fedha 2023/2024, wameweza kukusanya mapato ya ndani bilioni 2.1 (2,101,175,191) ikiwa ni asilimia 74.57 ya makadirio ya kukusanya kiasi cha bilioni 2.81(2,817,631,000).

“Tunakubaliana na Mkuu wa Wilaya, na tutafuata maagizo yake ya kuona halmashauri tunafikia malengo ya ukusanyaji mapato,kwanza tutahakikisha tunawasimamia watendaji, na wanasimamia na kukusanya mapato, lakini pili, Mtendaji wa Kata atakaeshindwa kukusanya mapato sisi kama halmashauri, hatushindwi kumuweka mwingine kwenye nafasi hiyo,” amesema na kuongeza kuwa

“Katika robo ya tatu zaidi ya kata 14 zimefanya vizuri, zimekusanya mapato kwa zaidi ya asilimia 100, huku kata sita ndiyo zikiwa zimekusanya chini ya asilimia 50,hivyo ni kuona kuna jitihada zinafanyika na kama tutaendelea hivi tutakusanya mapato kwa zaidi ya asilimia 100,”.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Ikupa Mwasyoge akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake

Mwasyoge amezitaja Kata zilizokusanya mapato kwa zaidi ya asilimia 100 ni Shagayu sh. 1,566,500 sawa na asilimia 418,Migambo 1,825,500 sawa na asilimia 332, Mtae sh. 2,237,496 asilimia 256 Mbaru sh. 759,500 asilimia 190.

Huku Kwekanga 3,391,400 sawa na asilimia 160,Ubiri sh. 1,102,500 asilimia 147, Ngwelo sh. 1,024,000 asilimia 137 na Mnazi sh. 3,232,200 asimilia 129.

Nyingine ni Hemtoye sh. 784,000 sawa na asilimia 125, Manolo sh. 2,377,300 asilimia 119, Lukozi sh. 6,705,000 asilimia 112, Mng’aro sh. 1,627,000 asilimia 108, Rangwi sh. 952,000 asilimia 106 na Magamba sh. 773,000 asilimia 103.

Wakati kata zilizokusanya mapato chini ya asilimia 50 ni sita, nazo ni Mbwei, Mbaramo, Gare, Ngulwi, Dule M, na Malibwi.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto