January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Lushoto awataka wananchi kuchagua viongozi wenye maadili

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto

MKUU wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Zephania Sumaye amesema pamoja na sifa na vigezo vilivyowekwa na Serikali katika kugombea uongozi wa Serikali za Mitaa, wananchi nao lazima wawe na vigezo vyao katika kuwapata viongozi waadilifu.

Amesema mtu anaefanya vitendo vya hovyo kwenye jamii ikiwa ni pamoja na kuchukua wanafunzi ama mabinti wa watu na kuwafanya wapenzi wake, huyo hafai kupewa uongozi. Hivyo, wananchi ni lazima na wao wachambue wagombea kutokana na vigezo vyao ili kupata viongozi bora.

Akizungumza Septemba 26, 2024, mara baada ya Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Ikupa Mwasyoge kutoa Maelekezo ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, Sumaye alisema mtu anaweza kuwa na vigezo vyote vilivyowekwa na Serikali, lakini akawa na vitendo vya hovyo kwenye jamii inayomzunguka.

“Pamoja na vigezo vilivyowekwa na Serikali katika kuwapata wagombea, lakini na ninyi wananchi mna haki ya kuwa na vigezo vyenu vya kumjua mgombea hasa kwa tabia zake binafsi. Mtu kama anachukua watoto wa watu, huyo hafai kuwa kiongozi. Lakini pia kiongozi awe na kazi ya kumuingizia kipato, asije akautumia vibaya muhuri wa Mwenyekiti wa Kijiji ili kujiingizia kipato” alisema Sumaye.

Msimamizi wa Uchaguzi, Mwasyoge akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa uchaguzi ikiwemo vyama vya siasa, amesema Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utafanyika Novemba 27, 2024. Zoezi la uandikishaji wa wapiga kura litafanyika kuanzia Oktoba 11 hadi 20, 2024 katika vituo vilivyopangwa, na Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji, na Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji utafanyika kwenye vitongoji na vituo vingine vilivyoelekezwa katika vijiji husika.

“Wakazi wote wenye umri wa miaka 18 au zaidi na waliokidhi masharti ya kisheria wanahimizwa kushiriki katika uchaguzi huu. Na wakazi wenye umri wa miaka 21 au zaidi wanaotaka kugombea nafasi za uenyekiti wa kijiji, ujumbe wa Halmashauri ya Kijiji, au uenyekiti wa kitongoji, anahimizwa kuchukua fomu za kugombea  katika Ofisi ya Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi.

“Fomu za kugombea zitatolewa na kutakiwa kurudishwa kuanzia Novemba Mosi hadi 7, 2024 kwa Msimamizi Msaidizi  wa Uchaguzi. Na uteuzi wa wagombea utafanyika Novemba 8, 2024. Muda wa kuweka pingamizi kuhusu uteuzi wa wagombea ni kuanzia Novemba 8 hadi 9, 2024, na uamuzi wa pingamizi utatolewa kuanzia Novemba 8 hadi 10, 2024, na rufaa zitapokelewa kuanzia Novemba 10 hadi 13, 2024, na uamuzi wa kamati ya rufaa utatolewa kuanzia Novemba 10 hadi 13, 2024” amesema Mwasyoge.

Mwasyoge ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, amesema kampeni za uchaguzi zitaanza Novemba 20 hadi 26, 2024, na zitafanyika kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 12 jioni.

“Ninatoa wito kwa wananchi wote wenye sifa kushiriki kikamilifu katika mchakato huu wa uchaguzi kuanzia hatua ya kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura, Hatua hii ya kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura ni hatua muhimu inayompa kila mwananchi mwenye sifa haki ya kisheria kushiriki uchaguzi kama mpiga kura au mgombea” amesema Mwasyoge.