November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Lazaro:Vyombo vya watumia maji msitumie fedha mbichi

Na Yusuph Mussa,Timesmajira Online,Lushoto

MKUU wa Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Kalisti Lazaro amevitaka vyombo vya Watumia Maji ngazi ya Jamii (CBWSO’s) visitumie fedha mbichi ambazo hazijawekwa benki, kwani kufanya hivyo kutaua miradi maji iliyopo vijijini ambayo haitakuwa endelevu.

Akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa wadau na watumiaji maji Wilaya ya Lushoto uliofanyika Mjini Lushoto, Lazaro amesema serikali inataka hadi Desemba, mwaka huu CBWSO’s zote ziwe zinaweka fedha benki kwa kutumia Mfumo wa Malipo ya Serikali wa GePG.

Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Wadau wa Maji wilayani humo

“Bodi za Maji zinatakiwa kusimamia mapato ya Serikali kwa kuhakikisha fedha zote zinaingia benki, badala ya watu kuanza kutumia fedha mbichi,tunataka mabadiliko kutoka 31 na kuwa saba, yalete tija kwa wananchi kwa kuweza kukusanya mapato na kuifanya miradi ya maji kuwa endelevu,”amesema Lazaro.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo amesema wanatoa uelewa kwa watumia maji ili waone umuhimu wa CBWSO’s huku nia yao ni kuviunganisha vyombo hivyo ili kufanya kazi kwa pana zaidi ili kuleta ufanisi.

Mhandisi Lugongo amesema ili kuwa na miradi endelevu inayotoa maji ni lazima kuwe na vyanzo vya uhakika vya maji, hivyo aliwataka wananchi kutunza mazingira huku akiwashauri madiwani, viongozi wa kata, vijiji, mitaa na vitongoji kuweza kuhamasisha wananchi na waone umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji.

Awali, akiwasilisha mada Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga amesema wilaya hiyo ina jumla ya wakazi 510,331, ambapo kwa Halmashauri ya Wilaya ya
Lushoto ina idadi ya watu 350,958 na Halmashauri ya Bumbuli watu 159,373 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Kati ya hao, watu 355,021 wanapata huduma ya majisafi sawa na asilimia 69.5 ya wakazi wote.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Lushoto Mhandisi Erwin Sizinga akizungumza kwenye Mkutano Mkuu wa Wadau wa Maji wilayani humo

Mhandisi Sizinga amesema miradi iliyopangwa kutekelezwa kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 ni miradi iliyopo kwenye kata 18 ikiwemo Lushoto Mjini, Usambara, Makole, Kwekanga, Funta, Mgwashi(Wanga), Vuga (Kiluwai), Shume (Gologolo), Hemtoye, Kisiwani, Kwai, Makanya, Ngulwi, Mahezangulu (Msamaka), Milingano, Kwemkomole, Mnazi (MkundiMbaru na
Mtae) na Lunguza (Tewe).

“Kutakuwa na miradi ya uchimbaji visima virefu katika Kata za Lushoto Mjini, Malindi, Makanya, Makole, Kwekanga, Kwai-Kwemakame pamoja na Mlola eneo la Chuo cha VETA ‘Survey’ na uchimbaji wa visima unategemea kuanza mwezi huu wa Oktoba,”amesema.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Tanga Mhandisi Upendo Lugongo (kushoto), mmoja wa viongozi walioshiriki kwenye Mkutano Mkuu wa Wadau wa Maji Wilaya ya Lushoto

Ambapo ameeleza kuwa miradi hiyo ina gharama ya kiasi cha zaidi ya bilioni 10.3 na ikikamilika itanufaisha wakazi 83,382 wanaoishi maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Lushoto ikiwa ni sawa na asilimia 16.3 ya wakazi wote wanaoishi Wilaya ya Lushoto.

Mhandisi Sizinga amesema, hadi kufikia Septemba, mwaka huu, Wilaya ya Lushoto imepokea sh. 2,443,502,496.88 kati ya 3,654,137,228. Hiyo ni sawa na
asilimia 66.9 ya fedha zote za bajeti kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024.

“Miradi hii ikikamilika itaongeza kiasi cha upatikanaji wa maji kwenye Wilaya ya Lushoto kutoka asilimia
69.5 ya sasa mpaka kufikia asilimia 85.8,” amesema Mhandisi Sizinga.

Wadau wa Maji Wilaya ya Lushoto

Mhandisi Sizinga amesema wamebadilisha muundo wa CBWSO’s, na sasa zitaundwa kwa kila tarafa, hivyo badala ya kuwa na CBWSO’s 31 sasa zitakuwa nane 8 kutokana na kuwa na Tarafa nane za Wilaya ya Lushoto ambapo sasa hivi zipo saba.