January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Kundya azindua kampeni ya kupanda miti Moshi

Na Martha Fatael,TimesMajira online,Moshi

SERIKALI wilayani Moshi imezindua kampeni maalum ya kupanda miti ya matunda na inayohifadhi mazingira katika maeneo ya kingo za mito katika eneo linalohudumiwa na Bodi ya Maji Bonde la Pangani (PBWB).

Kampeni hiyo imelenga kuotesha miti zaidi ya 1000 katika kijiji cha Shinga,Kata ya Uru Kusini wilayani Moshi vijijini kama njia ya kutunza mazingira ya mito iliyopo kijijini hapo sanjari na kutoa elimu ya wananchi kutofanya shughuli za kibinadamu katika kingo za mto.

Mkuu wa wilaya hiyo Alhaji Rajab Kundya,alitaka viongozi wa vitongoji na vijiji kuhakikisha wanasimamia na kulinda miti inayooteshwa ili iweze kuleta mabadiliko chanya kuhusu suala zima la mazingira na uhifadhi wa kingo za mito.

“Moja ya changamoto kubwa tunayokabiliana nayo kutokana na uharibifu wa mazingira unaosababisha kujaa kwa udongo kwa mito ni uwepo wa mafuriko baada ya mito kukosa uelekeo na hivyo kuvamia makazi ya watu”alisema Kundya.

Kwa upande wake, mhandisi mazingira kutoka PBWB, Arafa majid alisema kampeni hiyo itahusisha kuotesha miti katika Mito ya Umbwe, Rau, Chemichemi ya Dongi na ya Njoro kwa Mkamba.

Alitaka wananchi kuepuka shughuli za kibinadamu katika eneo la Mita 60 jambo ambalo huathiri mito husika na baadaye wananchi kupatwa na mafuriko na hivyo kukosa makazi na kuharibu miundombinu.

Nao baadhi ya wananchi wa Kijiji hicho wameomba serikali kuwachukua hatua za kinidhamu wenyeviti wa vitongoji na vijiji wanaoidhinisha mauzo ya ardhi kwa ajili ya makazi katika maeneo ya kingo za mito.

Mmoja wa wakazi hao, Joseph Macmililan alisema wananchi hawana uelewa kuhusu vipimo vya mita 60 zinazotajwa kisheria katika kingo za mito ama kufahamu maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya hifadhi za ardhi kwa matumizi ya umma na kutaka viongozi wawajibishwe wanapoidhinisha mauzo ya ardhi hiyo.