November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Korogwe awataka wafanyabiashara kulipa kodi

Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe

MKUU wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga William Mwakilema amewataka wafanyabiashara waendelee kulipa kodi kwa hiari sababu ndiyo uti wa mgongo wa taifa kwa shughuli za maendeleo na huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, maji na barabara.

Huku ikiitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuweka mazingira mazuri ya ulipaji kodi ikiwemo kutoa elimu kwani wakati mwingine wafanyabiashara wanashindwa kulipa kodi kwa vile hawajapata elimu.

Mkuu wa Wilaya ya Korogwe William Mwakilema akizungumza kwenye mkutano wa wafanyabiashara Korogwe. Wengine ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Korogwe Mwanaid Adadi (kushoto), Katibu wa CCM Wilaya ya Korogwe Vijijini Safina Nchimbi (kulia), na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wilaya ya Korogwe Rajab Kamili (wa pili kulia).

Ameyasema hayo Juni 3, 2024 kwenye mkutano ulioandaliwa na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Wilaya ya Korogwe, na kumualika Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya kusikiliza changamoto zao, uliofanyika ukumbi wa Halmashauri ya Mji Korogwe.

“Tanzania yetu itajengwa na sisi wenyewe, hakuna mtu mwingine atatoka nje kuja kuijenga,Serikali haina shamba, shamba lake Serikali ni wananchi wake ambao wanafanya biashara wanalipa kodi,hata vitabu vitakatifu, walimuuliza Yesu Kristo, ni halali kulipa kodi kwa Kaisari!,”

“Akawaambia hebu nipeni hiyo sarafu, ina chapa gani, wakasema ina chapa ya Kaisari, akawaambia ya Kaisari ambaye ndiyo Serikali, mpeni Kaisari, na ya Mungu mpeni Mungu,kwaio sisi tuendelee kumuabudu Mungu aliyetuweka na tumtumikie, lakini Serikali tunawajibu sisi tunayoitumikia tuweze kulipa kodi za halali ili iweze kujiendesha na kutuletea maendeleo kwenye nchi yetu” amesema Mwakilema.

Mwakilema amesema, wananchi wa Halmashauri zote mbili za Korogwe, zile za Mkoa wa Tanga na nyingine nchini.wakiungana kwenye kulipa kodi, ndipo wataweza kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye suala la shughuli za maendeleo na kupeleka huduma za kijamii.

Meneja wa TRA Wilaya ya Korogwe Evason Lushaka akitoa ufafanuzi wa baadhi ya mambo kwenye mkutano wa wafanyabiashara

Akijibu risala ya wafanyabiashara, Mwakilema amesema wamepokea maombi yao, na kwa vile wanataka Serikali ipate, na wafanyabiashara wapate, basi wataona namna ya kuboresha mazingira ya wafanyabiashara na wasiweze kufunga maduka yao kwa mtaji wao kukata kutokana na kulipa kodi kubwa.

Akisoma taarifa ya wafanyabiashara, Mweka Hazina wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wilaya ya Korogwe Hamis Kaniki amesema moja ya kero za wafanyabiashara ni kuwa na makadirio tofauti kati ya TRA Wilaya na Mkoa, kukadiriwa kodi kubwa kuliko uhusika wa mtaji wa biashara na makadirio ya mapato ya kila mwaka ya mfanyabiashara.

“Usumbufu wa TRA kwenye kodi ya mauzo, ‘Service Levy’ inachukuliwa kwenye mauzo, ambapo inakula faida na mtaji wa mfanyabiashara, mfanyabiashara kutakiwa kulipa madeni ya kodi ya miaka 10 hadi 15 iliyopita kama vile TRA na halmashauri hawakuwepo kwa miaka hiyo ya nyuma.

“Ushauri, TRA Wilaya na Mkoa visomane katika kukadiria kodi ndani ya mwaka mmoja wa fedha, makadirio ya kodi yazingatie uhalisia wa mtaji, waondoe usumbufu katika kodi ya Service Levy ichukuliwe kwenye mauzo ili isiwaumize wafanyabiashara, ama ilipwe pamoja na malipo ya leseni ya kila mwaka” amesema Kaniki.

Mweka Hazina wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Wilaya ya Korogwe Hamis Kaniki akisoma risala ya wafanyabiashara kwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe William Mwakilema

Meneja wa TRA Wilaya ya Korogwe
Evason Lushaka akizungumza na mwandishi wa habari mara baada ya mkutano huo, amesema wamekuwa wanatoa elimu ya mlipa kodi mara kwa mara kwa kuwatembelea kwenye kata zao na kusema suala la kupishana makadirio kati ya Mkoa na Wilaya inatokana na baadhi ya wafanyabiashara kuwa wadanganyifu.

“Makadirio tunayafanya ofisini, lakini tunapotembelea kwa wafanyabiashara, wakati mwingine tunakuta tofauti, bahati nzuri, tofauti hiyo hainekani na TRA Mkoa tu bali timu ya Mkoa inapofika wilayani, inazunguka na waliopo wilayani na kuona tofauti iliyopo kati ya makadirio ya awali na uhalisia wa biashara husika,” amesema Lushaka.

Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga Wilfred Tumba amesema changamoto na kero zote za wafanyabiashara wamezichukua kwani nyingine ni za kisera, na nyingine ni za uelewa, ambapo wataendelea kutoa elimu.

Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Tanga Wilfred Tumba akitoa ufafanuzi wa baadhi ya malalamiko ya wafanyabiashara wa Korogwe

Pia amesema hakuna tofauti ya kusoma makadirio kati ya Wilaya na Mkoa, na kinachotakiwa kufanywa na wafanyabiashara ni kubadilisha taarifa zao kutokana na mwenendo wa biashara zao.