December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu

Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe

MKUU wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga William Mwakilema amewataka viongozi wa vijiji na vitongoji kwenda kuwatumikia wananchi kwa uaminifu na uadilifu kwa kuhakikisha wanaondoa changamoto zinazowakabili ikiwemo migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji.

Ameyasema hayo Disemba 21,2024 wakati anafunga mafunzo ya siku mbili yaliyotolewa kwa viongozi wapya wa vijiji na vitongoji kwenye Tarafa ya Mombo yenye kata 10,vijiji 45 na vitongoji zaidi ya 250. Mafunzo hayo yaliandaliwa na Afisa Tarafa ya Mombo Alex Mhando kwa gharama zake, huku akichangiwa na wadau ili kukamilisha mafunzo hayo yaliyofanyika mjini Mombo.

“Nendeni mkawe waadilifu na waaminifu kwa wale wananchi waliowapa dhamana ya uongozi. Wananchi wamewaamini, hamkujiweka wenyewe sababu ilikuwa ni uchaguzi, na wagombea walikuwa ni wengi, lakini miongozi mwao, ninyi ndiyo mmepata dhamana ya kwenda kuwatumikia wananchi, hivyo mkawe waadilifu na kutenda haki kwa wananchi ili kuwaletea maendeleo yao.

“Kwa kutenda hayo niliyosema, shughuli za kiuchumi na kijamii zitakwenda kuimarika katika maeneo mbalimbali ikiwemo suala la mifugo, kilimo na biashara ambazo ndiyo shughuli kuu wananchi wanakwenda kuzifanya. Kwenye suala la kilimo na mifugo ni jambo linafanya sisi viongozi tutoke ofisini na kutumia muda mwingi kwenda kwa wananchi kusuluhisha. Ninyi viongozi kutokana na mafunzo mliyopewa, mkawe chachu ya kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji” alisema Mwakilema.

Mwakilema, pia alimuagiza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Mwanaamina Mruma kwenda vijijini kuandaa Mpango wa Matumizi Bora wa Ardhi, na kama mpango huo tayari ipo basi ufanyiwe utekelezaji ili kuona migogoro ya ardhi inapungua kama sio kumalizika kabisa.

Awali, Afisa Tarafa wa Mombo, Mhando, alimueleza Mkuu wa Wilaya sababu ya yeye kuandaa mafunzo hayo, kwani akiwa Afisa Tarafa, na anapokwenda vijijini kusikiliza kero za wananchi, amebaini baadhi ya viongozi wa vijiji, vitongoji na watendaji hawajui sheria, kanuni na taratibu ikiwemo maadili ya uongozi.

“Kutokana na ziara mbalimbali za vijiji nilizokuwa nikizifanya mara kwa mara kwenda kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi katika maeneo yao, yapo mambo niliyaona kwa baadhi ya viongozi katika Serikali zetu za vijiji na baadhi ya watendaji ambayo ni mapungufu ya kutojua baadhi ya sheria, taratibu, kanuni na maadili ya kuongozi.

“Nikaona kama Afisa Tarafa ni vyema kutokana na Serikali hii mpya ya vijiji iliyoingia madarakani sasa pamoja na viongozi wengine wote wa vijiji na kata wa chama na Serikali ambao wanashirikiana wote kwa pamoja katika kusimamia na kuongoza katika maeneo yetu, tuwe na Semina Elekezi kwa siku mbili kwa viongozi wote wa vijiji na kata kama inavyofanyika kwa viongozi wengine kwa kuwajengea uwezo na Utawala Bora” alisema Mhando.

Akifungua mafunzo hayo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Muhidini Mnkande alisema viongozi wa vijiji waliochaguliwa ambao karibu wote ni kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanatakiwa kwenda kufanya kazi iliyotukuka na kutoa imani kwa wananchi kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 kuichagua CCM.

Mnkande aliwataka wenyeviti wa vijiji wasitumie ubabe kuongoza kwa kuwatisha watendaji wa vijiji. Ni lazima kila kiongozi ajue mipaka yake ya uongozi, na kufanya kazi kwa kushirikiana na kupendana, kwani ndiyo kutafanya waweze kuwatumikia wananchi na kuweza kusimamia kwa pamoja shughuli za maendeleo kwenye vijiji vyao.