Na Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Korogwe
MKUU wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga William Mwakilema amesema, pamoja na uchache wa watumishi kwenye hospitali ya Wilaya hiyo ameitaka huduma zitolewa kwa muda wote wa saa 24.
Amesema kuna wakati yeye na Mkuu wa Polisi (OCD) Wilaya ya Korogwe wanatembelea vituo vya kutolea huduma usiku kama wananchi wa kawaida huku wakikuta baadhi ya watumishi hawapo, hivyo amewataka wmwanaopangiwa zamu za usiku waweze kuwepo kwenye vituo vyao vya kazi.
Mwakilema ameyasema hayo Machi 6, 2024 kwenye uzinduzi wa majengo manne ya Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, Makuyuni ambayo ni wodi ya upasuaji wanawake, wodi ya upasuaji wanaume, jengo la upasuaji (theatre) na jengo la kuhifadhia maiti.
“Majengo tunayo na vifaa tunavyo lakini pamoja na upungufu wa wataalamu aliosema Mganga Mfawidhi wa Hospitali maelekezo yangu ni tuwajibike kazini ili tuweze kuwahudumia wagonjwa wanapokuja hapa hospitali,”.
Mwakilema amesema hataki kumuwajibisha yeyote kutokana na doria aliyofanya usiku wala watu kujua alikwenda wapi na wapi, anachotaka ni uwajibikaji kwa wahudumu wa afya kuona wanatenda haki kwa kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Kwa hiyo Mkurugenzi (Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Goodluck Mwangomango) uendelee kufanya hiyo kazi. Kama Mganga Mfawidhi, DMO (Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Miriam Cheche) na wasaidizi wako wote hakikisheni mnafanya wajibu wenu ambao mmekasimiwa,”amesema Mwakilema.
Awali akisoma taarifa, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, Makuyuni Dkt. John Petron amesema hospitali hiyo ni miongoni mwa 67 za kimkakati zilizojengwa nchi nzima.
Ambapo jumla ya majengo 22 yalitarajiwa kujengwa yakigharimu kiasi cha bilioni 7.5 kwa makisio ya mwaka wa fedha 2018/2019 na mpaka sasa 14 ndiyo yamejengwa.
“Fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi awamu ya kwanza ilipokelewa mwishoni mwa Oktoba 2018 na ilianza na majengo saba ikiwemo ya wagonjwa wa nje (OPD), huduma ya maabara,mionzi, wazazi, bohari ya dawa, kufulia na utawala.ambago yamegharimu kiasi cha bilioni 1.8.
“Awamu ya pili ya ujenzi, fedha ilipokelewa Mei, 2021 na iliendelea na majengo matatu ambayo ni jengo la watoto, jengo la wodi ya wanaume na jengo la wodi ya wanawake wagonjwa mchanganyiko ambayo yamegharimu milioni 500,” amesema Dkt. Petron.
Dkt. Petron amesema awamu ya tatu ya ujenzi, walipokea milioni 800 kwa ajili ya jengo la kuhifadhia maiti, jengo la huduma ya upasuaji, jengo la wodi ya upasuaji ya wanaume na jengo la upasuaji ya wanawake na ujenzi umekamilika huku kiasi cha milioni 31 zimebaki, ambapo sh. milioni 13 ni ya matazamio.
Sanjari na hayo ameeleza kuwa hospitali hiyo ilianza kutoa huduma rasmi Juni 30, 2020 kwa kuanza na huduma za wagonjwa wa nje na kuendelea kuongeza wigo wa kutoa huduma kwa kadri miundombinu ya kuwezesha kutoa huduma ilipokuwa ikiongezeka.
Ambapo mpaka sasa wagonjwa 18,912 wamehudumiwa Wamama waliojifungua ni 1,036 miongoni mwao 75 walijifungua kwa njia ya upasuaji.
Amesema kutokana na upanuaji huduma mbalimbali na upatikanaji wa dawa, hospitali imeweza kuongeza ukusanyaji wa fedha za papo kwa papo kutoka sh. 5,274,100 mwaka wa fedha 2020/2021 hadi kufikia sh. milioni 58 mwaka 2022/2023, na mwaka huu wa fedha (2023/2024), hadi kufikia Februari, 2024, wamekusanya sh. milioni 58.
Pia amesema changamoto zinazoikabili hospitali hiyo ni upungufu wa watumishi kwa asilimia 79 kwani mahitaji ni 200 waliopo ni 42 sawa na asilimia 21.
Hata hivyo, Halmashauri imeendelea kuwasilisha maombi ya kupewa watumishi wa sekta ya afya katika Ofisi ya Rais- TAMISEMI katika bajeti ya mishahara kila mwaka.
Changamoto nyingine ni ukosefu wa kichomea taka,njia tembezi za kupitisha wagonjwa (walk ways), ukosefu wa gari la wagonjwa (ambulance), kwani gari linalotumika sasa ni chakavu na linahitaji matengenezo makubwa na ya mara kwa mara ambayo hospitali haiwezi kumudu.
Vilevile vyombo vya kuhifadhi maji (matenki), hasa wakati huu ambao huduma za kulaza wagonjwa zimeanza kutolewa, upungufu wa nyumba za watumishi, na kukosekana uzio kwa ajili ya ulinzi na usalama katika eneo la hospitali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mwangomango amesema mpaka sasa Serikali imetoa kiasi cha bilioni 3.1 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya hospitali hiyo, na kusema baadhi ya kazi zinazotakiwa kufanywa ni pamoja na ujenzi wa vyoo vya nje na jengo la kupumzikia wanaouguza wagonjwa.
“Pia zipo milioni 600 kwa ajili ya vifaa tiba kwenye zahanati na vituo vya afya, na tupo kwenye hatua za manunuzi. Tumepata magari mawili mapya, moja ambulance (Kituo cha Afya Bungu), na gari Ofisi ya DMO,” amesema Mwangomango.
More Stories
Madaktari wa Tanzania, Comoro waanza kambi kwa kishindo
Watakiwa kushirikiana kutikomeza matatizo ya lishe
CCBRT yazidi kuunga mkono juhudi za Rais Samia