Na Yusuph Mussa, TimesMajira Online, Njombe
MKUU wa Wilaya ya Njombe mkoani Njombe Kissa Kasongwa amewapa hadi Oktoba 30, mwaka huu Kiwanda cha Chai cha Ikanga Tea Company Ltd kilichopo Tarafa ya Lupembe wawe wamelipa malimbikizo ya malipo ya chai kwa wakulima ya sh. milioni 250.
Aliyasema hayo Julai 27, 2022 kwenye mkutano wa wadau wa chai Tarafa ya Lupembe, ambapo alisema hawawezi kuendeleza zao hilo kama baadhi ya wakulima watakuwa wanadai malipo yao.
“Haturidhiki na mwenendo wa baadhi ya wawekezaji sababu wanasababisha malalamiko kwa wakulima. Ofisa Kilimo (Simon Chatanda), zungumza na wawekezaji sababu Lupembe tumeshuka katika uzalishaji wa zao la chai kutokana na malalamiko ya wakulima.
“Tulipe madeni na kuondoa malalamiko ya wakulima, Lupembe itarudi namba moja kwa uzalishaji wa chai Tanzania. Meneja wa Kiwanda cha Ikanga (Mohamed Kasira), umeahidi utaanza kulima wakulima Agosti 6, mwaka huu ukianza na sh. milioni 50. Na hadi Oktoba 30, mwaka huu utakuwa umemaliza deni la sh. milioni 250 wanazodai wakulima… naomba iwe kweli” alisema Kasongwa.
Kasongwa ambaye kwenye mkutano huo alikuwa anamuwakilisha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe Waziri Kindamba, ambaye sasa anakwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, alisema Serikali imedhamiria kufufua zao la chai kwa kuboresha kilimo cha chai ikiwemo mbegu bora za vikonyo, kuandaa mazingira mazuri ya kilimo ikiwemo pembejeo.
Kasongwa alisema suala la mbolea limekuwa na changamoto kutokana na UVIKO 19 na vita ya Urusi na Ukraine, hivyo ukiacha kuwa ghali, hata upatikanaji wake umekuwa mgumu, na hiyo ni kutokana na nchi nyingi zenye uchumi mkubwa kuigombania.
“Lakini kutokana na changamoto hiyo, Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara nchini Burundi, alitafuta muwekezaji wa kujenga kiwanda cha mbolea mkoani Dodoma, na leo hii kiwanda hicho kimeanza uzalishaji wa mbolea ambayo hata ninyi wakulima wa chai Lupembe mtapata mbolea hiyo kwa bei nafuu” alisema Kasongwa.
Meneja Mkuu wa Ikanga Tea Company Ltd Kasira alisema wakulima wa chai Tarafa ya Lupembe wanapoteza sh. bilioni 4.7 kwa mwaka kwa kushindwa kuandaa mashamba yao kwa ubora unaotakiwa.
Afisa Mradi Mwandamizi wa Mradi wa Agricon Boresha Chai wa Shirika la IDH Michael Joseph alisema wapo kwenye mapinduzi makubwa ya kuhakikisha zao la chai linaleta tija kwa wakulima wa Tarafa ya Lupembe.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa