Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Kilindi
MKUU wa Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga Hashim Mgandilwa amesema jitihada zinahitajika katika ukusanyaji wa Mapato ya ndani ili kuweza kufikia lengo la ukusanyaji mapato kwa asilimia 100.
Amesema mwaka 2023/2024, Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi ilivuka lengo la ukusanyaji mapato kutoka kwenye makisio waliyojiwekea ya sh. 2,248,333,500, na kuweza kukusanya sh. 3,128,796,832 sawa na asilimia 139.
Amesema hayo Februari 12,2025 kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025.
“Ili kuweza kufikia malengo ya ukusanyaji tunatakiwa tuongeze jitihada kubaini vyanzo vyote vya ukusanyaji mapato. Mwaka jana (2023/2024) tulivuka malengo ya ukusanyaji mapato, lakini kwa mwaka huu hadi robo ya pili (Desemba 31, 2024) tupo asilimia 46.4 (sh. 1,357,124,411)” amesema Mgandilwa.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/img-20250213-wa00383664100724024626378-1024x449.jpg)
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi Idrissa Mgaza aliweka msisitizo kwenye makusanyo ya mapato ya ndani kwa kusema hakuna senti itaachwa katika ukusanyaji wa mapato hayo.
“Tuwe makini kwenye ukusanyaji mapato ili tuweze kukusanya mapato vizuri.
Mkurugenzi (Mtendaji wa Halmashauri, John Mgalula), weka vizuri timu yako ili kuhakikisha kila chanzo cha fedha kinachopita kwenye wilaya hii kinakusanywa,”amesema Mgaza.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/img-20250213-wa02795088401502433286143.jpg)
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilindi Mohamed Kumbi amewataka madiwani kwenda kuwasaidia watendaji wa kata na vijiji kukusanya mapato na waache kuwahurumia wananchi kuwa wakilipa mapato watateseka.
“Twendeni tukakusanye mapato kwa kuwasaidia watendaji wa vijiji na kata. Na msije mkawazuia wananchi kuwa wakilipa mapato watateseka…tuache hilo” amesema Kumbi.
Akijibu hoja ya mapato, Mkurugenzi Mtendaji, Mgalula alisema wamejipanga kuona wanafikisha asilimia 100 ya makusanyo ya Mapato ya Ndani ifikapo Juni 30, mwaka huu.
Mgalula amesema timu ya kukusanya mapato imejipanga vema, ambapo wameweza kuongeza mashine 100 za ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki (POS), huku wakiwa 46 za zamani, hivyo kufanya kuwa na POS 146. Lakini pia wameweza kununua gari Pick Up kwa ajili ya kushughulikia ukusanyaji mapato kwenye masoko, magulio na minada.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/img-20250213-wa02815627626321799386217.jpg)
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mara baada ya kikao, Mgalula alisema wana matumaini makubwa ya kufikia malengo ya ukusanyaji mapato wa sh. 2,922,270,928 kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
“Mwaka wa fedha 2023/2024 makisio yetu ilikuwa sh. 2,248,333,500, na kuweza kukusanya sh. 3,128,796,832 sawa na asilimia 139. Mwaka huu 2024/2025 tuliongeza makisio ya mapato hadi sh. 2,922,270,928, na hadi robo ya pili Desemba 31, 2024 tumekusanya sh. 1,357,124,411 sawa na asilimia 46.4.
“Naamini hadi Juni 30, mwaka huu, tutaweza kufikia asilimia 100 ya ukusanyaji mapato, kwani wananchi wetu wanatarajia kuvuna mazao yao ikiwemo mahindi hivi karibuni, hivyo hadi Juni 30, hatutaweza kufikia makusanyo ya asilimia 139 kama yale ya mwaka jana, lakini malengo ya kukusanya asilimia 100 yatafikiwa,”amesema Mgalula.
![](https://timesmajira.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/img-20250213-wa02824633466408979652500.jpg)
More Stories
Rais Samia kufanya ziara ya kikazi Addis Ababa nchini Nigeria
Serikali ipo kwenye maandalizi ya TASAF III,ambao hawajainuka kiuchumi TASAF II kupewa kipaumbele
Bil.51 zachochea kasi ya maendeleo Manispaa Tabora