Na Martha Fatael,Timesmajiraonline,Same
SERIKALI imetaka vikundi vya vijana wanawake na wenye ulemavu kutotumia fedha za mikopo kwa ajili ya kujipongeza kwani kwa kufanya hivyo ni kujiandaa kushindwa kurejesha mikopo husika.
Mkuu wa wilaya ya Same, Kasilda Mgeni amesema hayo wakati akikabidhi mikopo yenye thamani ya Sh Mil 183,500,000 kwa vikundi 34 vya miradi ya aina mbalimbali wilayani humo.
Amesema kitendo Cha kutumia fedha kwa malengo yasiyokusudiwa ni kukwamisha juhudi za serikali katika kuwakomboa wananchi na lindi la umasikini jambo ambalo ni kinyume na maelekezo ya serikali.
Aidha Mkuu wa Wilaya ametaka vikundi hivyo kuboresha mitaji yao pamoja na kurejesha fedha kwa wakati ili kuruhusu vikundi vingine kukopa zaidi.
Kasilda ametaka halmashauri ya wilaya hiyo kutoa namba ya akaunti za marejesho ya fedha hizo ili kuwarahisishia wanavikundi kurejesha bila usumbufu.
Awali mkuu wa divisheni ya maendeleo ya jamii wilayani Same, Charles Anatoly amesema vikundi vingi viliomba mikopo lakini nyenye sifa ni 34 pekee huku vilivyoachwa katika awamu nyingine ni vingi zaidi.
Amesema fedha hizo ni za mwaka Jana na kwamba Bado halmashauri Ina fedha za kutosha kutoa mikopo huku alitaka vikundi kujitokeza kuomba mikopo hiyo.
Ametaka wanavikundi kuwatumia maafisa maendeleo ya jamii katika kusajili vikundi ili kuhakokisha vinafuata Taratibu za kisheria katika kuepuka udanganyifu na upotevu wa fedha za serikali.
Kwa upande wao baadhi ya wanavikundi wamesema fedha hizo zitasaidia pia kuweka amani ndani ya familia zao.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi