Na Mwandishi wetu ,Timesmajira Online,Mbeya
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbeya Vijijini imempongeza Mkuu wa Wilaya ya Mbeya,Solomon Itunda, kwa kusimamia vyema utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya wilaya hiyo.
Pongezi hizo zilitolewa wakati wa ziara ya kamati hiyo iliyolenga kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi. Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbeya Vijijini, Akimu Mwalupindi, alisema miradi yote waliyotembelea imeonekana kuwa katika hatua nzuri na inatekelezwa kwa viwango vinavyoridhisha.
“Miradi yote tuliyoipitia leo ipo vizuri. Tunakupongeza Mkuu wa Wilaya ya Mbeya kwa usimamizi mzuri wa miradi hii ya maendeleo,” amesema Mwalupindi.
Katika ziara hiyo, Kamati ya Siasa ilikagua ujenzi wa Shule ya Amali, ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita moja kuelekea Hospitali ya Wilaya ya Inyala, pamoja na utekelezaji wa mradi wa tenki la maji Itewe na miradi ya umeme katika Kata ya Mshewe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo Solomon Itunda ameshukuru kamati hiyo kwa ushirikiano na ushauri walioutoa, akiahidi kutekeleza maelekezo yote ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kuwanufaisha wananchi.
Ziara hiyo ni sehemu ya utaratibu wa CCM wa kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Ilani ya Chama kwa lengo la kuhakikisha thamani ya fedha za umma inazingatiwa na miradi inatekelezwa kwa ufanisi.


More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama