December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Baadhi ya vitanda mbalimbali vya kisasa vilivyotolewa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Sadeline Health Care, Sara Kitainda ili kusaidia huduma za afya Wilayani Iramba. Mpigapicha Wetu

DC Iramba alipongeza shirika la Sadeline Health Care

Na Seif Takaza,TimesMajira Online,Iramba

MKUU wa Wilaya ya Iramba Mkoani Singida,Emmanuel Luhahula ameipongeza Shirika la Sadeline Health Care kwa kutoa msaada wa vitanda 21 katika wodi ya akina mama vyenye thamani ya zaidi ya sh.milioni 32.

Akizungumza wakati akipokea msaada wa vitanda hivyo kutoka kwa shirika hilo lenye makao makuu yake Jijini Dar es Salaam katika hafla fupi iliyofanyika nje ya jengo la Halmashauri hiyo mjini hapa alisema kuwa msaada huo utasaidia sana katika sekta ya afya.

Baadhi ya vitanda mbalimbali vya kisasa vilivyotolewa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Sadeline Health Care, Sara Kitainda ili kusaidia huduma za afya Wilayani Iramba. Mpigapicha Wetu

“Mkurugenzi wa Sadeline, Sara Kitainda nakushukuru sana kwa msaada huu, nina uhakika kuwa vitanda hivi vitawasaadia akina mama sehemu ya kulala ili wajifungue vizuri katika Hospitali yetu.

“Lazima turudishe shukrani kwenu maana kitendo hii kinatufariji sana, na tunatoa wito kwa wasomi wote walioko kwenye taasisi mbalimbali kuendelea kuiunga mkono Wilaya yetu kwa kujitolea misaada mbalimbali” amesema.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanavitunza vizuri vitanda hivyo ili viweze kuihudumia jamii kwa muda mrefu.

“Niombe Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha mnavitunza vizuri vitanda hivi ili vifanye kazi iliyokusudiwa kwa sababu leo hii sisi tupo kesho hatupo na tunatamani wanaokuja waendelee kufaidika na matunda ya vitanda hivi,” amesisitiza Luhahula.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sadeline Health Care, Sara Kitainda amesema kuwa vitanda hivi vimetoka katika shirika la Rotary Club toka Nchini Canada ambavyo vimegharimu takribani tsh.milioni 32.3 .

“Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, leo hii nimefarijika sana kukukabidhi vitanda 21 kwa ajili ya kusaidia kutoa huduma za Afya katika Hospitali yetu ya Kiomboi ili akina mama waweze kujufungua wakiwa mahali salama,” amesema Kitainda.

Hata hivyo Kitainda aliongeza kuwa lengo la taasisi yao ni kusogeza huduma katika Wilaya hii hivi karibuni kwa kuanzisha tawi la taasisi hiyo.

“Natoa wito kwa wadau mbalimbali kuungana nasi katika jitihada za kutoa huduma mbalimbali katika wilaya yetu. Taasisi yetu inatarajia kufanya kampeni ya kuhamasisha wananchi kupima tezi dume kwa njia ya kisasa pamoja na kupima shinikizo la damu bure” amesema.

Halikadhalika, Sara ametoa wito kwa wataalam mbalimbali wa afya ikiwemo waliokwisha staafu hususan walioko nje ya nchi na ndani ya nchi ambao ni wazaliwa wa Wilaya hii kutoa ushirikiano wa dhati kusaidia Wilaya hii kwa shughuli mbalimbali za maendeleo.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Dkt.Adam Mashenene ameishukuru taasisi hiyo Sadeline Haelth Care na kuahidi kutoa ushirikano pindi taasisi hiyo itakapoka fungua tawi lake Wilayani Iramba.

Hata hivyo Dkt.Mashenene ameahidi kivutunza vitanda hivyo kwa manufaa ya jamii kwa ujumla ili viweze kutoa huduma kwa muda mrefu.

Taasisi ya Sadeline Health Care imekuwa na utaratibu wa kuchangia vifaa vya huduma za afya ambapo mwaka juzi ilitoa vitanda 18 na hivi karibuni Taasisi hiyo inatarajia kutoa mashuka Wilayani hapa.