November 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Ilemela ahimiza kero za wananchi zipatiwe ufumbuzi

Na Judith Ferdinand, TimesMajira, Online Mwanza

MKUU wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masalla, amemtaka Mtendaji wa Kata ya Buswelu,kuwapanga watendaji wake pamoja na kukaa na wenyeviti wake wa mitaa,ili waanze kutatua changamoto ambazo zimetajwa na wananchi wa kata hiyo.

Masalla, ametoa mwito huo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Buswelu, ikiwa ni mwanzo wa ziara yake ya awamu ya pili ya kata kwa kata wilayani humo kwa lengo la kukagua shughuli za maendeleo, kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO-19, kusikiliza kero na changamoto za wananchi na kisha kuzipatia ufumbuzi.

Masalla,amesema, katika kutatua changamoto za wananchi, wenyeviti wa mitaa, watendaji wa mitaa na kata wana wajibu wa kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu.

Amesema watendaji hao wanalipwa mishahara na Serikali, hivyo ni muhimu wakasimama kwenye mstari.

“Ni muhimu mtendaji wa kata hiyo, akae na watendaji wake na wenyeviti wa mitaa yake watatue changamoto ambazo wananchi wamezitataja, kwani nyingi zipo ndani ya uwezo wao,”amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masalla, akizungumza na wananchi wa Kata ya Buswelu,ikiwa ni mwanzo wa ziara yake ya awamu ya pili ya kutembelea kata kwa kata wilayani humo ya kukagua utekelezaji wa shughuli za maendeleo, kuhamasisha wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya UVIKO-19, kusikiliza keri na changamoto za wananchi na kisha kuzipatia ufumbuzi uliofanyika shule ya msingi Buswelu.picha na Judith Ferdinand.

Amesema wafanye mikutano na watu wao wawaelekeze nini cha kufanya, wakifanya hivyo hawatamlaumu diwani, Mkuu wa Wilaya, Mbunge wala Mkurugenzi maana mkurugenzi anayo ya kwake ya kufanya.

“Dhima ya Serikali na kazi iliotuweka hapa ndio hii, kwa hiyo ukae na watendaji wako na wenyeviti wako anzeni kutatua changamoto ambazo zimetajwa hapa,kwa sababu nyingi zipo kwenye uwezo wenu,zile ambazo zimeshindikana tuwe na kazi ya kuwasiliana kwa Mkurugenzi cheza na ofisi yangu,kwa Mkurugenzi kukilegalega mimi wajibu wangu ni kumkumbusha nini cha kufanya,”amesema Masalla na kuongeza;

“Pia amesema kuna maeneo mtendaji huyo akifanya wao hawataingilia hata kama watu watalalamika, yeye akisikia watu wamepigwa faini kwa sababu ya uchafu atampongeza na atamwambia Mkurugenzi ampandishe cheo kwa sababu atakuwa amesima kwenye mstari.”

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa kata hiyo walimuomba Mkuu wa Wilaya hiyo kuwasaidia changamoto mbalimbali zinazokabili ikiwemo kero ya daladala kukatisha safari, barabara,maji,umeme na migogoro ya ardhi.