Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline, Ileje
MKUU wa Wilaya ya Ileje, mkoani Songwe, Farida Mgomi, uamuzi wa Serikali kuanzisha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ni kuona maisha ya walengwa yanaimarika na kinyume na hivyo inasikitika.
DC Mgomi alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki katika Kijiji cha Yuli kilichopo katika Kata la Mlale wilayani hapa wakati akizungumza na wananchi wakiwemo wanufaika wa Mpango wa TASAF, ambapo changamoto kubwa ambayo amesikia kwa maelezo ya wanufaika ni kuwa wale waliondolewa kwenye TASAF wamekata tamaa kiasi cha kushindwa kuendelea kwenye vikundi.
“Naomba hapo mnisikilize vizuri ili tuelewane vizuri, kwanza Serikali haipo kwa ajili ya kufanya mwananchi anungunike, bali kuboresha maisha yake.
Serikali inapokuwa na mipango yake, mipango yote ina muda wa kutekelezwa, inawezana ikawa na mpango wa miaka kumi au mitano na lazima iwe na malengo,” alifafanua DCMgomi na kuongeza;
” Kwa hiyo mpango wa TASAF ina muda na malengo yake kama ilivyo kwenye mipango mingine ikiwemo elimu.”
DC Mgomi alizidi kutoa ufafanuzi kuhusu mipango ya Serikali, akitolea mfano elimu akisema mpango wa Serikali ni mtoto wa shule msingi asome miaka saba na baada ya hapo ahitimu na akifanikiwa kufaulu aendelea na sekondari.
“Kwa hiyo tunategemea baada ya kipindi cha miaka saba mtoto afaulu na kujiunga na sekondari ambako atasoma na akifaulu ataendelea na chuo kikuu,” alisema na kusisitiza;
“Hakuna elimu ya chuo kikuu ya miaka kumi, elimu ya chuo kikuu ni miaka mitatu, minne na mitano, hivyo na mpango wa TASAF una muda wake.
Kama ulikuwa kwenye TASAF kwa miaka tisa lengo ni kuboresha kaya za walengwa, lengo kama lilikuwa nikuboresha maisha kwa miaka tisa mtu ameshindwa kuboresha maisha yake sasa hapo nani atalaumiwa?” Alihiji Mgomi.
Alisema kwa Serikali ni masikitiko makubwa kama waliamua kumuingiza mtu kwenye mpango kwa miaka mitatano akashindwa kuboresha maisha.
Alifafanua kuwa kwa kipindi hicho wanatarajia mlengwa awe ameanzisha miradi kama vile ufugaji kuku, awe anafuga mbuzi na nguruwe kama ameshindwa maana yake hapo Serikali inabakiwa na masikitiko.
Tathmini zilizofanywa TASAF zimeonesha kuwa kaya takribani 400,000 kwenye mpango huo zinaweza kujimudu kiuchumi, hivyo kustahili kuondolewa kwenye mpango ili kutoa nafasi kwa wananchi wengine wenye sifa kuingizwa kwenye mpango huo.
Hata hivyo, walengwa wengi kwenye mpango huo hawataki kuhitimu kwa hiari kwa lengo la kutaka kuendelea kupokea ruzuku inayotolewa na Serikali kupitia TASAF.
Baadhi ya wanufaika wa TASAF wanaipongeza Serikali kwa kuanzisha mpango huo ambao umewakomboa kiuchumi na hadi kuomba kwa hiari yao kuondolewa kwenye mpango huo.
Mmoja wa wanufaika aliyeomba kuhitimu kwa hiari yake Mkazi wa Kijiji Ipililo, Kata ya Ipililo, Halmashauri ya Wilaya Maswa, mkoani Simiyu, Esther Hoja Dome (49) aliwataka wanufaika wenzake kutumia ruzuku wanayopewa kuanzisha miradi ili waweze kujiletea maendeleo kama ambavyo amefanya yeye.
“Hii hela ukiichezea maendeleo hayatakuwepo kwako, utakuwa na maisha magumu moja kwa moja, lakini ukijitaidi na kutafakari ufanye nini, utapata maendeleo.”
Ushauri huo ulitolewa na mnufaika wa TASAF alipokuwa akieleza mafanikio aliyopata tangu alipojiunga na TASAF.
Anasema japo watu wanaopewa ruzuku ya TASAF na kulalamika kuwa ni ndogo, lakini yeye alipoanza kulipwa ruzuku hiyo aliidunduliza baadaye kulinunua mbuzi wawili, akawa ameanza ufugaji.
Kwa mujibu wa Esther, mbuzi hao walipokuwa wakizalishana aliuza, ambapo mbuzi mmoja mkubwa alimuuza sh. 150,000 na baadaye alijikuta amepata mtaji akaanzisha biashara ya kuuza vitenge.
Mbali na kuuza mbuzi na kupata mtaji wa vitenge kiasi cha sh. 200,000, lakini leo umeongezeka na kufikia sh. 500,000. Aidha, anasema mbuzi nao wameendelea kuzaliana, ambapo wamefikia 11, huku wengine akiendelea kuwauza.
More Stories
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa
Dkt. Kazungu atembelea miradi ya umeme Dar es Salaam