Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Chunya
SERIKALI Wilayani Chunya mkoani Mbeya imevitaka Vyama vya Ushirika wilayani humo kulima mazao ya Mahindi na Alizeti ili kujiongezea kipato kupitia uzalishaji huo .
Kauli hiyo imetolewa Mei,14 ,2025 na Mkuu wa wilaya ya Chunya,Mbaraka Alhaji Batenga wakati akifungua rasmi kiwanda cha kusaga Unga na kukamua mafuta ya alizeti kilichopo katika Kijiji cha Kalangali ambacho ni cha Chama Kikuu cha Ushirika cha wakulima wa Tumbaku Chunya (CHUTCU)
Mkuu huyo wa wilaya amesema kuwa kujikita Kwenye mazao hayo kutawaongozea wakulima kwakuwa soko la mahindi la uhakika lipo lakini faida itakayotokana na uzalishaji wa unga wa kutosha na kuuza huku akihimiza kuongeza juhudi ya kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa kiwandani hapo.

“Vyama vya msingi wekeni utaratibu wa kuona namna ambavyo mtalisha kiwanda hiki ili malighafi ziwepo maana kiwanda kina uwezo wa kufanyakazi masaa ishirini na nne hivyo kwa kuwepo malighafi za kutosha kutasaidia kiwanda kuzalisha kwa kiwango stahiki na hatimaye mtapata faida zaidi” ameongeza Batenga.
Akifafanua zaidi Batenga amesema kuwa wakulima wa vyama vya ushrika bado wana wajibu wa kuhakikisha wanamiliki ardhi kwaajili ya matumizi ya sasa na hata matumizi ya baadaye ya vyama hivyo kwani ardhi inaongezeka thamani kila siku
Mkuu wa wilaya ya Chunya Mhe Mbaraka Alhaji Batenga amewataka wakulima wa vyama vya ushirika wilaya ya Chunya kuhakikisha wanamiliki ardhi kwaajili ya matumizi ya sasa na hata matumizi ya baadaye ya vyama hivyo kwani ardhi inaongezeka thamani kila siku
“Hata ninyi wenyewe mnaongoza wakulima ambao wana ardhi hivyo hata ninyi vyama vya ushirika hakikisheni mnamiliki ardhi na mkishakuwa na ardhi hakikisheni mnatafuta hati, hakuna kitu kinatafutwa kwasasa kama ardhi, jambo hili ni muhimu sana hapo mbeleni. Wekeni ardhi hiyo salama kwakuikatia hati ili kiongozi atakayekuja na anauchu na ardhi asiweze kuitafuna” amesema Batenga
Mrajisi msaidizi wa vyama vya ushirika Mkoa wa Mbeya, Richard Edlia amesema ufunguzi wa kiwanda hicho ni tafsiri ya moja kwa moja ya Maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuongeza thamani mazao ya wakulima kwani kiwanda hicho ni moja kwa moja kitaongeza thamani ya Mahindi na alizeti za wakulima wa wilaya ya Chunya.
Awali akitoa taarifa za ujenzi wa kiwanda hicho, Fransisco Chidege amesema lengo la ujenzi wa kiwanda hicho ni kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima wa Mahindi na Alizeti wa wilaya ya Chunya kwa kupata eneo la kuuza mazao yao kwa bei nzuri jambo ambalo litaendelea kuwanufaisha na kuongeza uchumi wa mkulima mmoja mmoja na hatimaye uchumi wa Taifa kwa ujumla
Hafla ya ufunguzi rasmi wa kiwanda cha kusaga unga wa Mahindi na kukamua mafuta ya Alizeti kilichogharimu shilingi milioni mia nne sitini na saba imefanyika leo ambapo Mkuu wa wilaya ya Chunya alikuwa mgeni rasmi.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka vyama vyote vya msingi vilivyopo mkoa wa kitumbaku Chunya pamoja na wananchi wa karibu na eneo kilipo kiwanda hicho.

More Stories
Kukosekana kwa malezi bora,sababu inayochochea ndoa za utotoni
Kusuasua utekelezaji mradi wa maji ,Mbunge ataka hatua zichukuliwe
Prof.Ndakidemi ashauri selimundu itibiwe bure