Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
MKUU wa Wilaya ya Nyamagana Amina Makilagi,amewataka wananchi wa Kata ya Mahina, waendelee kuiamini na kuiunga mkono serikali ya awamu ya sita kwa jitihada zake za kuwaletea maendeleo na huduma bora.
Pia, amewaonya wasiruhusu siasa kuigizwa katika miradi ya kijamii ya sekta za afya,elimu na miundombinu ya barabara wanayoletewa na serikali.
Ametoa kauli hiyo wakati akihutubia wananchi wa mitaa ya Igelegele na Kagomu,Kata ya Mahina wilayani Nyamagana,katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Mahina Kati.
Amesema imani huzaa imani,hivyo wananchi na jamii ya Mahina waendelee kuiamini na kuiunga mkono serikali iwaletee maendeleo yatakayowawezesha kupata huduma bora.
“Nimekuja kuwaambia tumepokea mradi wa jengo la upasuaji katika Zahanati ya Mahina, ukikurupuka ukaanza bila kuwataarifu wenye mradi wakigoma utafanyaje,kazi yenu katika mradi huo mtachangia milioni 11.9,serikali na mfadhili watawaunga mkono kwa milioni 120,”ameeleza Makilagi.
Pia amesema mradi huo wa jengo la upasuaji na jengo la wagonja wa nje (OPD) inatekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) katika zahanati hiyo ili kuwaepusha na vifo watoto na wajawazito,wazee pia watatibiwa hapo na hivyo wachangamkie fursa maana ni mradi wao.
Mkuu huyo wa wilaya amesistiza mradi huo utawahudumia wananchi wote wana CCM na wa vyama vingine na wasio na vyama, hivyo wajitoe kuchangia na kushiriki ujenzi kwa kusaidia mafundi kusogeza mawe,matofali na kusomba maji si lazima wachangie fedha tu.
“Maendeleo yanaharibiwa na watu wenyewe na ninyi ndio mnafahamu adha mnayopata kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya,katika mradi huu mkiruhusu siasa ikaingizwa eti utampaisha Rais Samia katika uchaguzi, mtaukosa ama utaharibika,”amesema Makilangi na kuongeza
“Atakayeingiza siasa au kuukwamisha mradi huu huyo ni size yangu na anayetaka kuiona rangi yangu ajaribu,siku zote msaliti vitani au anayetoboa mtumbwi ili tuzame wote,huyo ni kumtosa safari iendelee,”.
Naye mkazi wa Igelegele na mmoja wasimamizi wa mradi huo,Zihaya Khalid,ameeleza kuwa wanufaika wakubwa ni watoto na wajawazito wanaopata changamoto ya kujifungua kwa njia ya kawaida,hivyo atawaelimisha wananchi na jamii umuhimu na faida ya mradi.
“Sisi akinamama lazima tujivune kupata mradi huu sababu utakuwa na manufaa kwetu kuliko watu wengine,wanaodhani hauna maslahi kwao nitawajibika kuwaelimisha na kuwahamasisha kujitolea tuukamilishe,”amesema.
Naye Mratibu wa TASAF Jiji la Mwanza, Peter Ngagani ameeleza kuwa serikali imewekeza zaidi ya milioni 120, mchango wa jamii zaidi ya milioni 11,ambapo mtaa wa Kagomu wenye kaya 1,788 kila moja itachanga sh.2,562 (4,580,000), kaya 2,238 za Igelegele sh.3,302 sawa na sh. 7,389,500.
Diwani wa Kata ya Mahina (CCM) Alphonce Francis aliwaasa wananchi wa kata hiyo waiunge mkono serikali kutekeleza mradi huo wa jengo la upasuaji,wachangie asilimia 10 kama moja ya masharti ya mradi na wamwombee Rais Dk.Samia kwa dhamira njema ya kuwaletea maendeleo.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua