Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeelezea nia ya kuendelea kuongeza vyanzo vya uzalishaji maji ikiwemo maji ya ardhini ili kuhakikisha inakidhi mahitaji ya wananchi wa Dar es Salaam na Pwani, sambamba na kudhibiti uharibifu na uchafuzi wa maji.
Hii ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa maji kupitia visima virefu pamoja na ujenzi wa Bwawa kubwa la kuzalisha maji la Kidunda, pamoja na ujenzi wa Mtambo wa kuzalisha maji wa Rufiji.
Hayo yamebainishwa na Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi DAWASA Ndugu Laston Msongole wakati wa ziara ya Bodi ya Wakurugenzi wa Wami/Ruvu kwenye mradi wa maji Kigamboni uliotekelezwa na DAWASA.
Amesema kuwa katika kukabiliana na mahitaji ya maji ya wananchi, Mamlaka inaendelea na kazi ya uchimbaji wa visima virefu zaidi kwenye Wilaya ya Kigamboni na kazi ya utafiti kubaini maeneo mengine yenye hazina ya maji ya ardhini yanayofaa kuhudumia wananchi.
“Tunashirikiana na Bonde la Wami/Ruvu katika kutafiti na kutunza vyanzo vya maji ya ardhini ambayo yameonekana yanaweza kutoa huduma kwa wananchi kwa zaidi ya miaka hamsini ijayo,” ameeleza.
Ameongeza kuwa kwa sasa mradi wa maji Kigamboni unazalisha lita milioni 70 kwa siku kutoka kwenye visima virefu 7 vilivyokamilika, ambapo wakazi wa Temeke, Chang’ombe na Kinondoni, na mpango uliopo ni kufikisha maji kwenye jimbo la Ukonga.
“Tayari zoezi la maunganisho ya maji kwa wateja limeanza, ambapo wateja 7,000 wameshaunganishwa na kazi inaendelea kufikia wananchi takribani 128,000 wa Kigamboni,” ameeleza.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bonde la Wami/Ruvu Mhandisi Elibariki Mmasi amesema kuwa Bonde la Wami/Ruvu kwa kushirikiana na DAWASA tunaendelea kufanya tafiti kwenye maeneo oevu ili kuhakikisha maji yaliyomo yanahifadhiwa na yaweze kutumika kutoa huduma kwa wananchi.
“Huu ni mkakati madhubuti wa kuhakikisha tunaongeza uzalishaji wa majisafi kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo maji ya ardhini ili miradi ya maji ambayo Serikali inawekeza fedha nyingi iweze kuleta tija kwa jamii inayokusudiwa,” ameeleza Mhandisi Mmasi.
Mbali na hapo tumejipanga na tunaendelea na jitihada za kudhibiti shughuli za kibadamu zinazofanywa kwenye safu za milima ya Uluguru inayotoa maji ya chemchem na maeneo ya mito inalindwa kikamilifu.
Ziara ya Wajumbe wa Bodi ya Wami/Ruvu kwenye mradi wa maji Kigamboni imeongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Bi Hafsa Mtasiwa.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa Â
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi