November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dawa za kulevya zamtupa jela mfanyabiashara Yanga miaka 30

Na Grace Gurisha,TimesMajira,Online, Tanga

MAHAKAMA Kuu, Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumu Kanda ya Tanga, imemuhukumu kifungo cha miaka 30 jela mfanyabiashara maarufu mkoani humo, Yanga Omary Yanga (Rais wa Tanga) baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya aina na herion zenye uzito wa gramu 1052.63.

Aidha, Mahakamani hiyo imemuachia huru, Mke wa Yanga, Rahma Juma na mfanyakazi wa wa ndani,Halima Mohamed baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.

Hukumu hiyo, imesomwa mwishoni juzi na Jaji Imakulata Banzi wa Mahakama hiyo. Kupitia hukumu yake amesema ametoa hukum hiyo kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka.

Jaji Banzi amesema amepitia ushahidi wa mashahidi saba na vielelezo 10, ambapo umeweza kuthibitisha bila kuacha shaka yoyote kuwa Yanga alikuwa akijihusisha na biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya.

Amesema kwa kuzingatia ushahidi huo, mahakama imemtia hatiani mshtakiwa (Yanga) kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya kama upande wa mashtaka ulivyomshtaki, ambapo atatumikia kifungo cha miaka 30 jela.

Jaji Banzi amesema upende wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shtaka hilo dhidi ya mkewe na mfanyakazi wa ndani kwa vile tangu mwanzo taarifa kuhusu kutendeka kwa kosa hilo zilitolewa zikimhusisha mshitakwa wa kwanza (Yanga).

ga, Yanga Omary Yanga maarufu kwa jina la Rais wa Tanga, akiwa amesimama katika kizimba cha Mahakama, baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, baada ya kupatikana na hatia ya kusafirisha dawa za kulevya.

“Mshtakiwa wa pili (Rahma) hakuhusishwa kwa namna yoyote tangu mwanzo na kwamba mshtakiwa wa tantu (Halima) alikuwa mfanyakazi wa ndani na vitu vilivyokutwa kwenye chumba chake vilithibitika havikuwa dawa za kulevya,” amesema Jaji Banzi

Kabla ya mahakama kutoa adhabu, upande wa mashtaka uliiomba mahakama kuzingatia uzito wa kosa na athari za dawa hizo ndani ya jamii na katika kuathiri uchumi wa nchi.

Wakili wa Yanga aliomba apewe nafuu katika adhabu yake kwa mshtakiwa kwa kosa ni kosa lake la kwanza na ana familia inayomtegemea.

Upande wa mashtaka katika kesi hiyo, uliongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi akisaidiana na Wakili Mwandamizi Pius Hilla, Mawakili wa Serikali Constantine Kakula, Salimu Msemo, Donata Kazungu na Mseley Mfinanga, ambaye ni mwanasheria mwandamizi kutoka Mamlaka ya Kuzuia Dawa za Kulevya (DCEA).

Washtakiwa katika shauri hilo walikuwa wanawakilishwa na Mawakili Majura Magafu, Nehemia Nkoko, Mohamed Kajembe, Kahoza Nicholaus na Adenis Tumaini. Kwa mujibu wa mashtaka, washtakiwa hao wanatuhumiwa kutenda kosa hilo, Oktoba Mosi,2018, maeneo ya Bombo jijini Tanga.