January 5, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dawa za kulevya kilo milioni 1.965 zakamatwa

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Kudhibiti Kupambana na Dawa za Kulevya imekamata kilogramu milioni 1.965 za aina mbalimbali za dawa za kulevya huku watuhumiwa 10.522 nao wakikamatwa katika kipindi cha Januari hadi Disemba 2023.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma,Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu Jesta Mhagama amesema kuwa kati ya watuhumiwa hao  wanaume ni 9,701 na wanawake ni 821

Amesema, jumla ya hekari 2,924 za mashamba ya bangi na mirungi ziliteketezwa huku ikielezwa kuwa  kiasi cha dawa za kulevya kilichokamatwa katika kipindi cha mwaka mmoja pekee ni kikubwa zaidi kuwahi kukamatwa hapa nchini kwani kinazidi kiasi cha kilogramu 660,465 zilizokamatwa katika kipindi cha miaka 11.

“ Aidha, Serikali imefanikiwa kuzuia uingizaji wa kilogramu 157,738.55 za kemikali bashirifu ambazo zingeweza kutumika kutengenezea dawa za kulevya kinyume cha sheria. “amesema Mhagama

Kwa mujibu wa Mhagama ,katika kuhakikisha jamii inapata uelewa juu ya tatizo la dawa za kulevya, Serikali imepanua wigo wa utoaji elimu kwa kuelekeza nguvu kwa wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo ambapo ,Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za  Kulevya imesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano (MoU) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kutoa elimu ya dawa za kulevya na rushwa kupitia klabu za kupinga rushwa nchini ambapo sasa zitaitwa  klabu za kupinga rushwa na dawa za kulevya.

“Tafiti zinaonesha kwamba, matumizi ya dawa yanaanza katika umri mdogo kati ya miaka 10 na 12 hivyo, Serikali imeona iweke mkazo huko kwani watoto wengi wanapitia katika shule hizo. “amesema

Pia amesema, elimu imeendelea kutolewa kwenye makundi mbalimbali ya kijamii yakiwemo ya  viongozi wa dini, viongozi wa kimila, waandishi wa habari, vyombo vya ulinzi na usalama, maafisa forodha na wakulima hasa katika maeneo yaliyokithiri kwa kilimo cha bangi na mirungi.

Kwa upande wa tiba amesema , Serikali imeendelea kuimarisha huduma kwa kuongeza vituo vya kutolea tiba kwa waraibu kwa kutumia dawa na huduma  za unasihi (MAT)  ambapo kwa mwaka 2023 kituo kimoja kimefunguliwa mkoani Morogoro katika gereza la kihonda ambapo hadi kufikia mwezi Disemba 2023, jumla ya vituo 16 vilikuwa vinatoa huduma kwa walengwa.

Aidha, vituo vingine viwili katika wilaya ya Muheza mkoani Tanga na Chalinze mkoani  Pwani vinatarajia kukamilika ifikapo mwezi Aprili mwaka huu huku akisema vituo vingine vitatu vitaanza kujengwa katika mikoa ya Shinyanga, Kilimanjaro na Pwani katika wilaya ya Mkuranga.

Aidha, serikali iko kwenye hatua za mwisho za ujenzi wa kituo kikubwa cha huduma za Tiba na utengamao (Rehabilitation centre) katika jiji la Dodoma ambacho mbali na huduma za matibabu pia yatatolewa mafunzo maalumu yatakayowawezesha waraibu kujitegemea kimaisha baada ya kukamilisha safari ya matibabu yao.

“ Aidha, kumekuwepo na ongezeko la waraibu wanaojiunga na tiba katika kliniki mbalimbali zilizopo nchini,sababu la ongezeko hilo ni kuadimika kwa dawa za kulevya mtaani baada ya kuvunja baadhi ya mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya ,“Takwimu kutoka kwenye vituo vya MAT zinaonesha jumla ya waraibu wapya 2,219 wamejiunga na tiba kwa mwaka 2023 na kufanya idadi ya waraibu wanaopata tiba ya Methadone kufikia 15,915. “alisema Mhagama na kuongeza kuwa

“Katika kuongeza ufanisi wa Mamlaka, Serikali imeanzisha kituo cha huduma kwa wateja ili kutoa nafasi kwa wananchi kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya.”

Vilevile amesema,serikali imekamilisha ujenzi wa maabara ya kisasa itakayotumika kwenye utambuzi wa sampuli mbalimbali za dawa za kulevya pamoja watu wanaotuhumiwa kutumia dawa hizo.