January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DART kushiriki kampeni ya Upandaji ‘MitiMilioni’ ya Benki ya NMB

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Taasisi ya Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (Mwendokasi) – DART wameungana na Benki ya NMB kupitia kampeni yao inayozidi kushika kasi ya Upandaji Miti Milioni kwa mwaka 2023, kwa kupanda miti 1,000 aina ya ‘Jacaranda’ katika ushoroba wa Bus Rapid Transit (Mwendokasi)

Zoezi hilo liliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya DART – Dkt. Florens Turuka akiambatana, Mkuu wa Wilaya Ubungo – Hashim Abdallah Komba, Mtendaji Mkuu wa DART Dk. Edwin Mhede na watumishi wa DART.

Kwa upande wa NMB, waliwakilishwa na Afisa Mkuu wa Wateia Binafsi na Biashara – Filbert Mponzi, Mkaguzi wa Ndani – Benedicto Baragomwa, Afisa Mkuu wa Technolojia na Mabadiliko ya Kidijitali – Kwame Makundi, Afisa Mkuu Utekelezaji – Ezekiel Herman pamoja na wafanyakazi kutoka Kanda ya Dar es Salaam.

Akizungumza katika zoezi hilo, Dkt. Mhede aliishukuru NMB kwa kuishirikisha DART katika kutekeleza maagizo ya Makamu wa Rais Dkt. Mpango ya kutaka mamlaka zote za Serikali, taasisi na mashirika ya umma kujikita katika kampeni hiyo inayolenga kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi.

“Shukrani NMB kwa wazo bunifu la kuja na kampeni hii, ambayo kwetu sisi DART ni fursa ya kutuwezesha kurejesha uoto wa asili katika ushoroba wa barabara zetu, ambao unaondolewa na ujenzi wake. Kampeni hii itatusaidia kurejesha uhalisia wa maeneo yetu”.

“Tumejipanga kuitunza miti hii, jukumu ambalo nalikabidhi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ulinzi wa Miundombinu ya DART (China-Tanzania Security), El-Malick Aboud, ambaye atashirikiana na watendaji wa mitaa, kata zinakopita na mradi wa mwendokasi kote Dar es Salaam.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Washauri ya DART, Florens Turuka, aliahidi kuwa miti hiyo 1,000 ambayo wataipanda kuanzia Ubungo kuelekea Kata za Manzese na Magomeni, wataitunza ipasavyo kama alivyosema Dk. Mhede, kwani lengo lao DART – ambao wanasafirisha abiria kupitia kauli mbiu ya ‘Usafiri wa Umma Nadhifu,’ ni kuitunza kwa asilimia 100.