January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Daraja lililokarabatiwa kwa milioni 40 lasombwa na maji,wanafunzi 100 wakatisha masomo

Na Moses Ng’wat,Timesmajiraonline,Mbozi.

DARAJA la mto Msambizi linalotenganisha vijiji vya Lusungo na Songwe katika kata ya Nanyala, Wilayani Mbozi ambalo miaka miwili iliyopita lilikarabatiwa kwa shilingi milioni 42 limesombwa na maji na kusababisha kukosekana kwa mawasiliano kati ya vijiji hivyo.

Hali hiyo imesababisha wakazi 20,000 wa kijiji cha Lusungo kukosa huduma mbalimbali za kijamii, huku wanafunzi 100 wa shule za sekondari wanaotoka katika kijiji hicho wamelazimika kukatiza masomo kwa muda kutokana na kutokuwepo kwa njia mbadala ya kuwafikisha kwenye shule wanazosoma ambazo ziko makao makuu ya kata hiyo katika kijiji cha Songwe.

Wakizungumza na waandishi wa habari, wananchi hao walisema kuwa, daraja hilo lilisombwa na maji wiki moja iliyopita baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha usumbufu mkubwa, huku wakiiomba serikali kuwajengea daraja la dharura ili kurejesha mawasiano.

Miongoni mwa wananchi hao, Faines Mbembela na Mpoki Kibona wote wakazi wa kijiji cha Lusungo walisema kukukatika kwa mawasiliano ya kijiji chao na makao makuu ya kata ambako huduma za msingi zinapatika imekuwa pigo kubwa kwao.

Hivyo, wameiomba serikali kuona uwezekano wa kurejesha mawasiano hayo kwa dhararua ili kuwaokoa na adha wanazozipata, ikiwemo hofu ya akina mama wajawazito kukosa hudumu muhimu pindi wanapotaka kujifungua.

Diwani wa kata hiyo ya Nanyala, George Msyani ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, alisema tayari uongozi wa kata umekutana na kufanya tathmini ili kujua mahitaji ya kiasi gani yanahitajika ili kuweza kurejesha huduma za mawasiliano ya usafiri katika daraja hilo.

“Tunapata hofi katika siku hizi ambazo serikali inafanya jitihada za kurejesha miundombinu muda ili kuwanusuru wanafunzi ambao kwa sasa hawaendi shuleni pamoja na watumishi wengine ambao hawataweza kufika katika maeneo yao ya kazi” alisema Msyani.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijiji na Mijini (Tarura) Mhandisi Robert Mwakitalima, alisema kuwa tayari wameshafanya tathmini ya gharama za kujenga daraja la dharura na kwamba ndani ya wiki moja mawasiliano ya daraja hilo yatarejea.

Aidha, Mhandisi Mwakitalima, alisema kuwa Tarura imeomba kiasi cha shilingi milioni 200 kwa ajili ya kujenga daraja la kudumu katika mto huo ikiwa ni mkakati wa kupata suluhisho la kudumu.