Na David John
WAKAZI wengi wa Jiji la Dar es Salaam wameitikia wito wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kwa kuvaa barakoa kama alivyoelekeza wiki iliyopita.
Katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam mwitikio wa uvaaji barakoa ulikuwa mkubwa tofauti na awali na wale ambao hawakuwa nazo, walilazimika kufunga vitambaa, hatua ambayo ilibadili mwonekano wa wakazi wa Jiji hilo ikilinganishwa na kabla ya kutolewa na agizo hilo.
Majira lilipita maeneo mbalimbali ya Jiji na kushuhudia idadi ndogo ya watu ndio waliokuwa hawakuvaa barakoa hususani kwenye daladala. “Huu mwaka wetu. Ni lazima tuongeze mapambano ya corona vinginevyo tutaisha,” alisema Emmanuel Jacob mkazi wa Kizuiani, Mbagala jijini Dar es Salaam.
Watu waliozungumzia uamuzi huo wa RC Makonda kutaka wananchi kuvaa barakoa, baadhi ya wananchi waliuunga mkono, japo walidai umetolewa ukiwa umechelewa, hivyo walitoa wito kwa mikoa mingine kuanza mara moja uvaaji wa barakoa.
Hata hivyo changamoto iliyojitokeza katika uvaaji wa barakoa, ni baadhi ya wananchi kujifunika pua zao kwa kanga, mitandio na kutumia muda mwingi kushikilia pua, hali inayoonesha kwamba bado kuna changamoto.
Kwa upande wa wauzaji wa maduka wamekuwa na mwitikio mkubwa tofauti na ilivyokuwa awali. Mfanyakazi katika kampuni ya FMJ Hard Ware, Ibarahim Hamis alisema wanalazimika kuvaa barakoa ili kuitikia agizo la Mkuu wa Mkoa la kutumia barakoa hizo kujilinda na kulinda wateja wao.
“Hali imeshakuwa mbaya sana hivyo lazima wateja wetu wanapokuja kupata huduma kabla hatujawahudumia lazima tuhakikishe wamevaa barokoa na hii ni kwa ajili ya kujilinda na kuwalinda dhidi ya corona,”alisema Hamis.
Alisema kama mteja hana Barakoa basi anatakiwa kujifunga kitambaa puani ndipo waweze kumruhusu kupata huduma.
Katika maeneo ya Buguruni ambapo biashara ya Hard Ware inafanyika kwa wingi wahudumu wengi na wateja wao walikuwa wamevaa barakoa. Naye Daniel Mademe mkazi wa Tabata Segerea alisema yeye ni mteja ambaye alifika kwenye maduka hayo bila barakoa na kujikuta akinyimwa huduma.
“Nililazimika kutafuta barakoa ndipo niweze kuhudumiwa. Kwa kweli hali ilishakuwa mbaya lazima tuzingatie na kufuata maelekezo ya watalaamu wetu, lakini tukijifanya wajuaji tunaweza kupoteza maisha. Hivyo nashauri wananchi hasa mkoa wa Dar es Salaam tuzingatie maelekezo ya watalaamu wetu.”alisema Mademe.
More Stories
MSF ilivyojidhatiti kusaidia serikali katika utoaji wa huduma za afya
Prof.Muhongo awapongeza vijana 32 waliotembea kwa miguu kutoka Butiama hadi Mwanza
Rais Samia atimiza ahadi Hanang