December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile

Dalili za wagonjwa Corona utata mtupu

Ni dalili zilizojitokeza kwa wagonjwa nchini kutofautiana na wale wa nje NIMR yaagizwa kufanya utafiti

Na Mwandishi Maalum, WAMJW

WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeitaka
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) kufanya
utafiti kuhusu ugonjwa wa Corona (Covid-19) kwa kuwa kuna tofauti
kubwa ya dalili zilizojitokeza kwa wagonjwa hapa nchini ukilinganisha
na wagonjwa waliopo nje ya nchi.

Agizo hilo limetolewa jana na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile, wakati
alipokutana na watafiti wa taasisi hiyo wakijadili maambukizi ya
ugonjwa wa Corona na aina ya matibabu ambayo wagonjwa wanatakiwa kupatiwa hasa baada ya kubainika kuwa dalili za ugonjwa huo zinatofautiana na dalili za wagonjwa wa mataifa mengine.

“Kuna mambo mengi ambayo tunapaswa kuyafanyia utafiti wa kisanyansi, moja ni uelewa wa jamii, tunataka kujua wagonjwa wanaougua Corona ni wagonjwa wa namna gani, wana magonjwa ya aina gani, dalili zinazowapata wagonjwa ni za aina gani.

Hapa tunataka tupate uelewa,” alisema Dkt. Ndugulile. Pia, alisema
kupitia utafiti huo wanataka kujua aina za matibabu ambayo wagonjwa
wanatakiwa kupatiwa ili kuhakikisha ugonjwa wa Covid-19 unadhibitiwa
hapa nchini.

Dkt. Ndugulile akiwa kwenye picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Yunus Mgaya pamoja na watafiti wa taasisi hiyo baada ya kumalizika kwa mkutano huo.

“Kutokana na muitikio mkubwa wa tiba asili na tiba mbadala, kupitia
kikao hiki nawaelekeza wataalamu wetu wajipange kufanya utafiti na
kutoa majibu ya tiba ya maambukizi ya virusi vya Corona,” alisema Dkt.
Ndugulile.

Alisema wamekubaliana na watafiti hao kufanyia kazi maagizo hayo ndani ya muda mfupi na kutoa majibu sahihi ambayo yatasaidia katika
mapambano ya ugonjwa wa Corona.

Waziri wa Afya, Dkt. Ndugulile akifafanua jambo baada ya kumalizika kwa mkutano kujadili jinsi ya kupambana na Covid-19 nchini. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Prof. Yunus Mgaya.

Naye Mkurugenzi Mkuu  wa NIMR, Prof. Yunus Mgaya alisema mapambano dhidi ya ugonjwa Covid-19 ni vita ambayo inapaswa kufanyiwa utafiti ambao utasaidia kupatikana kwa njia sahihi za kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huo.

“Tunafahamu kwamba jamii za kiafrika zina utaalamu katika miti shamba. Katika hili kuna tafiti mbalimbali zinaendelea ili kuchunguza uwezo wa miti shamba kwa lengo la kupunguza makali ya Covid-19.