January 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CWT Igunga yatoa vyandarua 200 sekondari ya Ziba

Na Lubango Mleka, Times majira oniline, Ziba – Igunga.

CHAMA Cha Walimu Wilaya ya Igunga (CWT) kimetoa vyandarua vya kujikinga na Mbu waenezao Malaria 200 kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Ziba baada ya bweni lao kuteketea kwa moto wiki hii.

Akikabidhi vyandarua hivyo kwa uongozi wa shule hiyo, Mwenyekiti wa CWT Igunga Mwl.Eliasi Mganda amesema kuwa, walipokea kwa masikitiko janga hilo la moto lililokumba bweni la wavulana shule ya sekondari ya Ziba, hivyo wakaamua kufanya jitihada za haraka kutoa vyandarua hivyo 200 kwa kushirikiana na Katibu wa Chama Cha Walimu Tanzania Mkoa wa Tabora Condraus Stephen ambaye amechangia kiasi cha shilingi 300,000.

Aidha, ameuomba uongozi wa shule hiyo kuvitumia vyandarua hivyo kama ilivyokusudiwa ili wanafunzi hao wasishambuliwe na mbu waenezao Malaria huku akiwataka wanafunzi hao kutojisikia wanyonge na wapweke kipindi hiki walichopata matatizo bali wasome kwa bidii na kufaulu mitihani yao.

Sanjari na hayo amewaomba wadau mbalimbali kuungana na CWT na serikali ya Wilaya na Mkoa kutoa msaada wa mahitaji mbalimbali ambayo bado wanafunzi hao hawajayapata ili waendelee na masomo yao kama kawaida.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Balozi Dkt. Batilda Salha Burian amekabidhi magodoro zaidi ya 200 na mablanketi kwa wanafunzi 210 wa shule hiyo misaada iliyotolewa na CRDB Kanda ya Magharibi na kampuni ya ununuzi wa tumbaku ya Alliance One ya mkoani Tabora.

“Kwa sasa tunaweza kufanya ukarabati bwalo liliopo hapa ili liweze kutumika kama sehemu ya kulala kwa wanafunzi hawa, wakati serikali ikiangalia hatua zingine za kujenga bweni lingine,”amesema Buriani.

Aidha ametoa pongezi kwa viongozi wa serikali na vyombo vya ulinzi ngazi ya Mkoa na Wilaya ambavyo vimefanya kazi kutwa nzima kuhakikisha wanafunzi hawa wanapatiwa msaada ili kuendelea na masomo.