January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi CUF Taifa, Juma Khalaga, wakati wa uzinduzi wa mchakato wa uchaguzi wa CUF kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.

CUF yapuliza kipenga rasmi kuelekea Uchaguzi Mkuu

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online

Chama cha Wananchi (CUF) kimepuliza kipenga cha uchaguzi ndani ya chama na kutoa ratiba kamili ya kura za maoni ambapo kimesema mgombea atakayetoa rushwa akibainika Baraza Kuu litamuondosha katika kinyanganyiro.

Pia kimekaribisha chama chochote chenye dhamira ya dhati kitakachotaka washirikiane kuelekea Uchaguzi Mkuu mwaka huu

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi CUF Profesa Ibrahim Lipumba alipowasili ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Omar Hamis Othuman. Picha na Hadija Bagasha Pemba.

Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi CUF Taifa, Juma Khalagai ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa mchakato wa uchaguzi wa CUF kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020.

Amesema kuwa, wanachama wote wenye sifa wajitokeze kwa wingi kuwania nafasi za kukiwakilisha chama katika Uchaguzi Mkuu 2020 ambapo wamewahakikshia kuwa chama hakina wagombea wateule.

”Ratiba yetu imeanza leo kwa zoezi la kuandaa fomu za wagombea na inatarajiwa kuhitimishwa tarehe 27,7, 2020 ambapo wagombea urais wa tiketi ya CUF wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar watateuliwaa,”amesisitiza.

Ameongeza kuwa, katikati ya tarehe hizo kutakuwepo na matukio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuandaa kura za maoni katika ngazi za kata na wilaya kwa Tanzania Bara na jimbo kwa Zanzibar.

Amesema, wanatarajia kuweka wagombea udiwani, uwakilishi wa ubunge, lakini pia watasimamisha wagombea urais wawili mmoja akisimama kwa ajili ya urais Zanzibar na mwingine atasimama kwa ajili ya urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa CUF Taif, Profesa Ibrahim Lipumba amepata mapokezi makubwa ya ujio wake visiwani Pemba ambapo Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Omar Hamis Othuman amesema hawana sababu ya kukishikia chama hicho silaha badala yake watahakikisha usalama wake unakuwepo katika kipindi chote atakachokuwepo huko.

Profesa Lipumba yupo Kaskazini Pemba katika ziara yake ya siku sita ya utelekezaji wa shughuli za chama kama sehemu ya kukiimarisha chama hicho katika kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu.

Profesa Lipumba amesema, watahakikisha wanasimamisha wagombea wa nafasi zote visiwani humo ikiwemo ubunge, udiwani na hata urais kupitia chama hicho kwani mkoa huo ni ngome ya CUF na wapo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi wote.

Katika ziara yake Profesa Lipumba amekabidhi kadi za chama hicho kwa vijana zaidi ya 100 watokanao na timu nne za mpira katika eneo la Micheweni ambapo ameahidi kuzipatia timu hizo jezi na mipira.