Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Iringa,
CHAMA cha Wananchi CUF kimesema endapo kitapata ridhaa ya kuongoza Serikali kutoka kwa wananchi kwenye uchaguzi wa Oktoba, mwaka huu, Chama hicho kitawekeza kwenye rasilimali watu ikiwemo afya na elimu.
Hayo yamesemwa na mgombea urais kupitia chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba wakati akihutubia wananchi wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa jana kwenye mkutano wake wa kampeni.
Amesema kama watu hawana elimu na afya bora, ukiwekeza kwenye vitu vingine haiwasaidia chochote. Mgombea urais huyo alisema Serikali ya CCM imekuwa ikiwekeza kwenye kununua vitu kama vile ndege badala ya kuwekeza kwenye miundombinu muhimu ya afya na elimu.
“Endapo tutapewa ridhaa Sera ya CUF itawekeza kwenye vitu muhimu vya afya na elimu ili viweze kuwasaidia Watanzania katika kujikwamua na umaskini,”amesema.
Kama Taifa, lazima tuwe na utaratibu wa kuhakikisha watoto wanapata lishe bora ili kujijengea kinga ya mwili na Serikali ina kila sababu ya kuhakikisha wanapata elimu bora.
Kuhusu Muungano, Profesa Lipumba amesema muungano ni muhimu na endapo watachaguliwa wataimarisha Muungano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar na pande zote kuwa na haki sawa.
Alisema watakapopata ridhaa hiyo ya kuongoza nchi wataendeleza muungano kwa kuwa ni muhimu kwa Taifa letu. Katika hatua nyingine mgombea urais huyo alisema Serikali ya CCM imeiacha njia panda sekta ya kilimo na bila kuleta mapinduzi ya kilimo.
“Bila kuleta mapinduzi ya kilimo viwanda haviwezi kuwepo, hivyo CUF inahitaji kuleta mabadiliko na mapinduzi katika sekta hiyo,”alisema Profesa Lipumba.
Alidai wanahitaji kuleta mabadiliko ili pawepo na mzunguko wa fedha, kwani wananchi wa Kilolo ni watu wanaojishughulisha na kilimo, lakini hawana msaada wowote wanaoupata kutoka Serikalini.
“Zamani Iringa ilikuwa kwenye mikoa minne iliyokuwa ikiongoza kwa uzalishaji mahindi, wananchi wa mkoa huu ni wachapa kazi, lakini hawajajengewa mazingira ya kuweza kuutokomeza umaskini,” alisisitiza mgombea urais huyo na kuongeza kuwa;
“Tunaomba kura zenu ili biashara zitoke na wananchi waweze kufanya biashara, uwekezaji uongezeke vitunguu vipate soko sio tu Tanzania, hadi Afrika Mashariki yote watu wapewe utaalamu wa kuweza kuongeza tija katika shughuli zao za kilimo.”
Hata hivyo alisema kuwa unapoongeza tija kwenye kilimo ndipo unapopata uwezo wa kuendeleza viwanda, kwani kilimo kinatoa chakula na endapo kilimo kikiwa na tija uzalishaji utaongezeka.
Kwa upande wake mgombea mwenza, Hamida Abdalah Huweishi amewataka vijana wasijutie kuzaliwa, kwani muda uliopita haukuwa muafaka, kwani CUF itaboresha kila sekta kwa kutumia rasilimali zilizopo.
“Vijana siyo taiFa la kesho ni Taifa la leo Sera ya Taifa la kesho ipo CCM na imewaweka kwenye uongo mtupu na kuacha rushwa itawale, pigeni kura CUF ili muyaone mabadaliko hamkuzaliwa kuja kuongeza idadi ya makaburi, CUF imedhamiria kuwainua,”amesema.
More Stories
The Desk & Chair yashusha neema Gereza la Butimba
TVLA,yapongezwa kwa kuzalisha chanjo
TAKUKURU,yasaidia kurejesha hekali 8