March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CRDB Grand Bunge Bonanza: Rais Samia Mgeni Rasmi, Wananchi Waalikwa

Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online – Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tamasha kubwa la michezo na burudani la CRDB – Grand Bunge Bonanza, litakalofanyika Jumamosi, Juni 21, 2025, katika viwanja vya Shule ya Sekondari John Merlini, Miyuji jijini Dodoma.

Bonanza hilo limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Bunge na Benki ya CRDB ambaye ndiye mdhamini mkuu na linabeba kaulimbiu isemayo: “SHIRIKI UCHAGUZI MKUU, KWA MAENDELEO YA TAIFA LETU”. na kulengakukuza mshikamano, afya na burudani kwa wabunge, watumishi wa serikali na wananchi kwa ujumla.

Akizungumza na waandishi wa habari Juni 18,2025 Bungeni jijini Dodoma Mwenyekiti wa Klabu ya Bunge Festo Sanga amesema,Michezo mbalimbali itashindaniwa ikiwemo mpira wa miguu, pete, kikapu, kuvuta kamba, mpira wa wavu, pamoja na michezo ya jadi kama bao na drafti. Burudani za muziki wa dansi, taarabu, ngoma za asili, ushairi na vichekesho pia zitapamba siku hiyo.

Amewaasa wananchi wa Dodoma wametakiwa kujitokeza kushuhudia bonanza hilo litakaloanza saa 1:00 asubuhi ambapo zawadi mbalimbali ikiwemo medali, tracksuit, jezi na kifungua kinywa zitatolewa kwa washiriki wote watakaofika kushiriki michezo hiyo.

Kwa mujibu wa Sanga , bonanza hilo linatarajiwa kuwa la kipekee kutokana na maandalizi kabambe, ushiriki mpana na uwepo wa viongozi wakuu wa kitaifa, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naye Mwakilishi wa Benki ya CRDB, Ntully Mwambapa, aliongeza kuwa bonanza hilo si tu burudani, bali ni njia ya kupongeza wabunge kwa mchango wao wa miaka mitano.

“Tunatambua nafasi ya michezo katika kuleta watu pamoja. Tunatoa wito kwa wakazi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi kushiriki,” alisema.

Aidha amesema ,Benki ya CRDB imedhamini bonanza hilo kwa kutoa msaada wa vifaa vya michezo vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 130, ikiwa ni sehemu ya kujenga afya, mshikamano na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika masuala ya kijamii.