September 19, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ubora wa wahasibu, wakaguzi kuimarika

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online DSM

BODI ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) imehitimisha mafunzo ya siku mbili yaliyokuwa yakiendelea Kwa wanaoisaidia Bodi katika Shughuli mbalimbali za mitihani ikiwa na lengo la kuboresha utungaji na usahihishaji wa mitihani kwa kuzingatia viwango vipya vya mitaala ili kuimarisha ubora wa wahasibu nchini.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo leo Septemba 12, 2024, Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) CPA Pius Maneno amewapongeza washiriki kwa kujitolea kujifunza mbinu mpya na teknolojia ambazo zitaisaidia Bodi katika Shughuli mbalimbali za mitihani

Aidha, amesisitiza kuwa umuhimu wa wataalamu hao kutumia maarifa waliyoyapata kusaidia wengine na kuboresha sekta nzima ya uhasibu nchini ili kuleta tija katika soko la Ajira duniani na kuchagiza katika ukuaji wa uchumi.

“Mmepewa nyenzo muhimu ambazo zitawasaidia kufanya maamuzi bora katika utungaji wa mitihani na usimamizi wa ubora, Tunahitaji ujuzi wa msingi na sio maarifa tu, ili kuwapata wahitimu wenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya soko la ajira, Hii inamaanisha tunajaribu zaidi vipaji na ujuzi kuliko maarifa ya nadharia pekee,” amesema CPA Maneno

Aidha, CPA Maneno amewataka kuwa mabalozi wa mabadiliko katika mitihani ya uhasibu, hivyo mitihani inapaswa kupima ujuzi halisi na sio kutumia teknolojia kama akili bandia (AI) inayoweza kutoa majibu ya nadharia, ambayo hayapimi uwezo wa mwanafunzi

Nakuongezea kuwa mafunzo haya ni muhimu kwa kuimarisha ubora wa wahasibu na kusaidia kutatua changamoto za ufaulu duni kwa wanafunzi.

Baadhi ya wanaoisaidia Bodi katika Shughuli mbalimbali za mitihani wameeleza kuwa mafunzo hayo yamewapa uelewa zaidi kuhusu usimamizi wa mitihani na mbinu bora za kujenga wanafunzi wenye uwezo wa kuhimili changamoto za soko la ajira kwa weledi wa kutosha na kusema kuwa mafunzo haya yamewapa mwanga mpya kuhusu changamoto zilizopo katika sekta ya uhasibu na namna bora ya kuzitatua.