Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online,Dar
KATIBU wa NEC, Itikadi Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, CPA, Amos Makalla Julai 15, 2024 ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Biashara na Usafirishaji (EACLC) unaoenda kugharimu zaidi ya bilioni 200 hadi kukamilika kwake.
CPA Makalla ametembelea na kukagua mradi wa jengo hilo unaojengwa kwenye eneo la stendi ya zamani ya mabasi ya mkoani, lenye vyumba vya maduka zaidi ya 2000, huku akisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaenda kuchochea uchumi wa nchi, kuongeza ajira, kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na China na kuongeza mapato katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo.
Amesema takribani ya miaka 10 mradi huo unaonekana kusuasua, hivi sasa unaenda kukamilika na utawasaidia wafanyabiashara wengi wazawa kutosumbuka tena kwenda china kuchukua bidhaa na badala yake watakuwa wakiagiza hapa ndani.
“Mwanzo wananchi hawakuwa na uelewa hususani wafanyabiashara, walidhani kuwa maduka haya zaidi ya 2000 yataenda kuwa ya hawa wenzetu wa China wakati si kweli isipokuwa yanaenda kuwa ya wazawa wa hapa ndani,”.
Mradi mwingine alioutembelea ni pamoja na Hospitali ya Sinza Palestina ambayo imeendelea kuboreshwa kutoka Kituo Cha Afya na hadi kufikia hadhi ya kuwa Hospitali ambapo hivi sasa ina uwezo wa kutoa huduma kwa mjamzito aliyetayali kwa kujifungua.
” Haya ni maendeleo, tukiangalia huko zamani tulikuwa na kale kajengo kadogo pale ( anaonesha kwa mkono) lakini Sasa hivi tumejionea wenyewe maendeleo yake haya makubwa na tumeambiwa hapa milioni 600 zimetolewa kwa ajili ya maboresho haya na hakika tumepiga maendeleo makubwa”, ameongeza Makalla.
CPA Amos Makalla, bado anaendelea na ziara yake ya kichama ya siku 10 katika Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo leo anaendelea na ziara hiyo Wilaya ya Kinondoni.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa