June 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CP.Wakulyamba awataka maofisa wa NCAA kuwa wabunifu

Na Mwandishi wetu, Timesmajira, Karatu

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Uhifadhi, Kamishna wa Polisi (CP) Benedict Wakulyamba, amewavisha vyeo Maofisa 22 na Askari watatu wa Jeshi la Uhifadhi la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) waliokamilisha mafunzo ya mabadiliko kutoka mfumo wa kiraia kwenda kijeshi.

Akizungumza katika hafla iliyofanyika Kituo cha Mafunzo Mbulumbulu mkoani Arusha, CP Wakulyamba amewataka wahitimu hao kuyaishi kwa vitendo mafunzo hayo kwa kufuata nidhamu ya kijeshi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.

Amesisitiza kuwa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ina imani kubwa na Jeshi la Uhifadhi katika kulinda rasilimali za Taifa, hivyo ni lazima kila mmoja afanye kazi kwa bidii, uadilifu na kuepuka vitendo vya rushwa.

Ameonya kuwa hatua kali za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayehusika na vitendo vya uhalifu au kushindwa kusimamia maadili ya jeshi.

Aidha, CP Wakulyamba amepongeza wahitimu kwa ubunifu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia katika kituo hicho, akisema ni utekelezaji wa agizo la Rais kuhusu kupunguza matumizi ya kuni na mkaa na kuhimiza taasisi nyingine za Wizara kuiga mfano huo.