NEW YORK, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema, janga la mlipuko wa virusi vya corona (COVID-19) limefanya macho yote ya Dunia kuelekezwa kwenye mtihani huo mkubwa zaidi ambao Dunia imekumbana nao tangu Vita vya Pili vya Dunia.
Guterres aliyabainisha hayo katika ujumbe wake maalum wa Siku ya Kimataifa ya Mama Sayari.
ìNi lazima tufanye kazi pamoja kuokoa maisha, kupunguza madhila na kupunguza madhara ya kiuchumi na kijamii kwani athari za virusi vya corona ni za sasa na za kutisha,”alieleza Guterres.
Alisema,mbali ya COVID-19 kuna janga jingine kubwa ambalo ni tatizo linaloikumba sayari ya Dunia ni la kimazingira.
ìBayoanuwai inaendelea kudorora, mabadiliko ya tabianchi yanafikia kiwango kisichoweza kudhibitika. Ni lazima tuchukue hatua kabambe za kuilinda sayari yetu kutokana na virusi vya corona na tishio la mabadiliko ya tabianchi,îalisema.
Aliongeza kuwa, janga la sasa ni kengele ya kutuamsha kufanya mabadiliko, kutojikweza na kutumia fursa kufanya mambo vyema zaidi kwa siku zijazo.
Kutokana na hali hiyo, Katibu Mkuu huyo alipendekeza hatua sita zinazohusiana na tabianchi, kama mwongozo wa kujikwamua na kazi tunayopaswa kufanya.
ìKwanza tunapotumia kiasi kikubwa cha fedha kujikwamua kutokana na virusi vya corona, ni lazima tufungue fursa mpya za ajira na biashara kwa hali ya mpito isiyo chafuzi.
“Pili panapotumiwa fedha za walipa ushuru kukwamua biashara, pazingatiwe upatikanaji wa ajira zinazojali mazingira na ukuaji endelevu,”alielekeza Katibu Mkuu huyo.
Jambo la tatu, Guterres alisema ni nguvu za kifedha zitumiwe kubadili uchumi kuwa unaojali mazingira na kuzifanya jamii na watu kuwa jasiri zaidi.
Aidha, jambo la nne alisema, fedha za umma zitumiwe kuwekeza kwa mustakabali, sio zama na ziende kwa sekta na miradi endelevu inayosaidia mazingira na tabianchi.
“Jambo la tano matishio ya tabianchi na fursa ni lazima vijumuishwe kwenye mifumo ya fedha, pamoja na nyanja zote za sera za umma na miundombinu. Na sita tunapaswa kufanya kazi pamoja kama jamii ya kimataifa,”alifafanua Guterres.
UNFPA
Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) limesema, linashikamana na wale wote wanaojitolea na kuwa katika mstari wa mbele kupigana na janga la virusi vya corona (COVID-19) kuanzia kwa wahudumu wa afya na wanaojitolea kusaidia bila malipo.
Shirika hilo limeeleza ni jambo la ujasiri kuwatunza wagonjwa, kwa madereva wa mabasi na wafanyakazi walio kwenye mstari wa mbele wa kupigana na janga hilo.
Pia linaendelea kuomboleza na wale ambao wamepoteza wapendwa wao katika janga hii kubwa zaidi la kiafya katika karne hii.
Kwa mujibu wa shirika hilo, licha ya changamoto zilizoletwa na virusi hivyo, wao wanaendelea kufanya kazi na serikali, washirika, mashirika ya Umoja wa Mataifa na wafadhili na inajiandaa kupigana na janga hilo.
Pia mipango ya kuendeleza biashara iko katika mstari wa mbele na kujitolea kwa hali na mali kuwahudumia wasiojiweza.
Aidha, UNFPA imebainisha kuwa, inafanya kazi na serikali na washirika wa kuweka kipaumbele katika mahitaji maalum ya wanawake na wasichana.
Kwa mujibu wa UNFPA,janga hilo la kimataifa linahitaji suluhu ya kimataifa, hivyo limetoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia wale wote walioathiriwa na janga hilo.
Chanjo
Mbali na hayo Umoja wa Mataifa umezindua juhudi za kimataifa za kutafuta chanjo ya virusi vya corona, wakati Rais wa Marekani Donald Trump akizusha mjadala kwa kudai kuwa wagonjwa watibiwe na kemikali za kuua vijidudu
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema, kulitatua janga hili kutahitaji mashirika ya kimataifa na viongozi wa Dunia kuungana na sekta binafsi kutengeneza na kusambaza chanjo ya virusi vya corona.
Hayo yalijiri siku moja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kusababisha ukosoaji mkubwa kutokana na pendekezo lake kuwa kemikali za kuua vijidudu zitumike kuwatibu wagonjwa.
“Kuna njia yeyote tunaweza kufanya kitu kama hicho, kwa kuingiza kemikali hizo mwili kwa kutumia sindano au kama kusafisha. Inaonekana kuwa kitu cha kupendeza kwangu,”Rais Trump aliwaeleza waandishi wa habari.
Aidha, Katibu Mkuu Guterres aliwaeleza viongozi wa taasisi na mashirika mbalimbali kuwa, Dunia inahitaji kuona utafiti, utengenezaji na usambazaji kwa njia ya usawa na mwafaka wa chanjo za COVID-19 pamoja na vifaa vya matibabu.
Wito huo ulikuja wakati ambao mjini Geneva,Uswisi Shirika la Afya Duniani (WHO) lilifanya mkutano wa video kuhusu ushirikiano wa kimataifa wa kutengeneza chanjo kwa pamoja na Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, Wakfu wa Gates na Muungano wa Kimataifa wa Utoaji Chanjo (GAVI).
More Stories
Kampeni msaada wa kisheria ya mama Samia kutatua kero za kisheria Katavi
Wizara ya madini yakusanya bil.521 nusu ya kwanza mwaka wa fedha 2024/25
Meya awafunda wenyeviti Serikali za Mitaa