November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

COSTECH, Afrika Kusini kushirikina
mradi wa afya na usalama wa chakula

Na Grace Gurisha, TimesMajira,Online,Dar

MKURUGENZI wa Kituo cha Uendelezaji na Uhaulishaji wa Teknolojia wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dkt. Gerald Kafuku, amesema wameungana na nchi ya Afrika Kusini kwenye mradi wa afya na usalama  wa chakula kwa lengo la kuwainua wabunifu wanaochipukia.

Dkt.Kafuku amesema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupitisha azimio la kuungana pamoja kwa ajili ya kuwainuia wabunifu hao.

Amesema mpango huo uliyopewa jina la Twiga pia una lengo la kuwainua na kuwatengenezea ajira, kwa hiyo nguvu hiyo ya pamoja pia itawasaidia kuwatafuta wabunifu sehemu mbalimbali hapa nchini.

Amesema mradi huo utakaowainua wabunifu wachanga watatu kutoka Tanzania na kwa idadi hiyo, ambapo kwa Afrika Kusini utagharimu sh. milioni 300.

Dkt. Kafuku amesema mradi huo utawasaidia vijana kuinua bunifu zao ambazo pia zitakuwa majibu ya changamoto mbalimbali nchini. Pia mradi huu utakuja na majibu ya changamoto za uhifadhi wa mazao yasiharibike.

Pia, Dkt. Kafuku ametoa wito kwa mbunifu yeyote mwenye wazo endelevu alipeleke COSTECH watamsaidia mtaji wa kuliendeleza mpaka kufikia hatua kubwa.

Mkurugenzi wa Kituo cha Uendelezaji na Uhaulishaji wa Teknolojia wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Gerald Kafuku akizungumza katika kupitisha aZimio la pamoja la kuwasaidia na kuwainua wabunifu wachanga na kuendeleza bunifu zao katika mradi wa afya na usalama wa chakula uliyopewa jina la Twiga wanaoshirikiana na nchi ya Afrika Kusini.

“Sisi hatuhitaji maneno mengi, mtu aandike tu jina lake na amebuni kitu gani sisi tutamsaidia na tupo nchi nzima kwa sababu tumeungana na Tamisemi, kwa hiyo hata mtu akienda kwenye ofisi yoyote ya Serikali wazo lake litatufikia COSTECH,” amesema Dkt.Kafuku 

Kwa upande wake, Meneja Mratibu wa mradi huo kutoka Afrika Kusini, Sina Legong amesema licha ya kubadilishana uzoefu wa nchi hizo kwenye bunifu mbalimbali pia itasaidia nchi hizo kupata wabunifu wenye uweledi.

Amesema kuwa miradi hiyo ni mwanga wa maendeleo kwa kuwa inaibua utatuzi wa changamoto mbalimbali kwenye jamii.

Naye mwakilishi wa Kampuni ya Pharmlinks, John Method amesema Kampuni yao inajihusisha na kuunganisha wauzaji wa dawa za binadamu kwa jumla na rejareja, kwa njia ya mtandao.

Amesema mradi huo, utawasaidia kukua na kuweza kufanya kazi kwenye mkoa wa Dar es Salaam kwa ukubwa zaidi na kwenye mikoa ya pembezoni wa nchi na kuweza kukuwa Afrika mzima. 

“Ubunifu wetu ni wa teknolojia inawarahisishia wale wauzaji rejareja kuweza kupata mizigo yao kutoka katika maduka ya jumla kwa urahisi zaidi kwa kutumia simu, kompyuta na tablet, hakuna haja ya wao kutembea muda mrefu kutoka walipo hadi kariakoo,” amesema.